Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema 1KORINTHO 15:33

KUJIKANA NDANI YA KRISTO YESU (sehemu ya tatu- Final)



Bro Jackobo


Utakuwa nami mpendwa katika kristo yesu
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com


Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu?? Karibu Tena kwenye sehemu hii ya tatu na ya mwisho ambapo ni muendelezo wa somo la Kujikana ndani ya Yesu ambapo tuliona maana ya kujikana ndani ya Yesu kristo, Tuliona nani alikuwa mwanzilishi wa kujikana tangu asili ambaye ni mfano wetu wa kuigwa tukaona na maeneo muhimu mawili ambayo mwamini anapaswa kuonyesha na kuthibitisha kuwa amejikana ndani ya Yesu kristo Yesu katika sehemu ya kwanza halafu tukasoma sehemu ya pili ambapo tuliangalia vipingamizi katika kujikana kwa mwamini mbele ya Mungu wake. Kama hujayasoma masomo hayo naomba uende uyasome ili upate mtiririko mzuri. Unaweza kubonyeza hapa ili usome πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Leo Tutaanzia kwenye kipengele cha madhara kwa kanisa kushindwa kujikana kikamilifu kwaajili ya kristo Yesu.


5. MADHARA KWA KANISA KUSHINDWA KUJIKANA KWAAJILI YA YESU KRISTO.
Mungu wetu ni wa utaratibu sana amabaye hawezi kumlazimisha mtu kumfuata bali anatamani kila mtu amfuate kwakuwa amependa kumfuata japo yeye Mungu sio kama mwanadamu ambaye ameweka uongozi wake usiwe wa mfumo wa kidemokrasia tu bali ameuweka uongozi wake wa theoklasia (Theocracy) ambapo ana utaratibu wake anaotaka tuufuate ambao una maelekezo ya kila kitu tunachotakiwa kukifanya na akaweka kwamba tusipofuata kuna madhara yatakayo tokea.

Sasa kanisa lazima likubali kufuata taratibu zake mwenyewe lasivyo madhara yatatupata kama ifuatavyo hapa chiniπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

A. Kutokujibiwa kwa maombi yetu
B. Kukosekana kwa matendo makuu ya Mungu
C. Kupotea kwa kibali na heshima mbele za Mungu

A. KUTOKUJIBIWA MAOMBI
Maombi ni mawasiliano ya pande mbili ambapo huwa mwamini anamuelezea yule anayemuamini juu ya yale yanamsibu na muaminiwa kutoa majibu kwa anayemuamini juu ya kile alichokiweka mezani. Kwahiyo maombi ni mchakato wa njia mbili ambapo lazima pande zote zipate muitikio kutoka kwa upande mwingine juu ya hoja moja inayowaunganisha ili kujenga uhusiano wa karibu sana "Intimacy".
Kwasababu ya kanisa kutokuwa na uhusiano mzuri na Mungu yani kushindwa kujitoa kikamilifu kwaajili ya Yesu kristo, mambo mengi yamemfanya Mungu azibe sikio lake lisiweze kusikia yale ambayo wanahitaji kwasababu hakuna lengo moja linalowaunganisha la kimahusiano. Sasa Mungu ndio maana anataka watu wake wote wajitoe kikamilifu na kama hawatajitoa wanakuwa wameikataa sheria yake na ndio maana anakuja kusema ya kwambaπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mithali 28:9 "Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo."

Pia ukifuatilia biblia utagundua wana wa Israel pale walipokosea mara nyingi waliingia katika mikono ya adui hata kupewa adhabu na Mungu mwenyewe. Sasa kipindi cha nabii Amosi wana wa Israel walikuwa wamekosea kiasi wakawa wanaabudu mpaka sanamu huku bado wakitaka kutaka kumfanyia Mungu ibada huku hawajajikabidhi kwa Mungu kikamilifu mpaka ikafika Mungu. Anakuja kufoka na kuwaambia maneno hayaπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Amosi 5:22-23 "Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu."

Kutoa kwao sadaka na kumfanyia Mungu nyimbo za shangwe za kuoyesha furaha yao kwa Mungu hakukuwa na maana kabisa mpaka Mungu akawa anawaambia wamuondolee nyimbo zao maana zimekuwa kelele kwakuwa mioyo yao haikuwa kwake kamili. Kwahiyo ukitaka Mungu akusikie lazima ujitoe kikamilifu mbele zake lasivyo utakuwa unajidanganya na utakuwa unapoteza muda wako. Hii inakuja kuthibitisha kile Mungu anataka kiuhalisia wakeπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 9:31 "Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo."

Sasa lazima pia uwe na moyo wa kutafakari kikamilifu sana na kwaakili ambayo imetulia sana kuelewa hili. Mungu amesema mwenyewe kabisa kwenye maandiko yake kuwa pale ambapo mtu anachagua kuishi katika dhambi huwa dhambi inamfarakanisha na Mungu na hata yale mambo anayokuwa anayaomba Mungu hawezi kuyajibu wala Mungu hawezi kuwaokoa maana dhambi inakuwa ni kiambaza kinacho watenganisha nyie na Mungu wenuπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Isaya 59:1-2 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; ]lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

B.. KUKOSEKANA KWA MATENDO MAKUU YA MUNGU.
Kanisa inapaswa kuwa ni sehemu ambapo madhihirisho makubwa ya uwezo wa Mungu kwa matendo makuu kuonekana lakini kwasasa imekuwa nii kitu ambacho ni adimu sana kwasababu watu wengi hawako thabiti sana mbele zake ili na yeye aweze kuyaonyesha matendo yake kwa kanisa. Kizazi hiki kimekuwa kina ukaidi sana hakiko tayari kabisa kujitoa kikamilifu kwaajili ya kristo kitu ambacho kinaleta mapooza ndani ya Nyumba ya Mungu na Mungu kumfanya anyamaze kabisa. Yesu alizungumza wazi kabisa kuwa kizazi hiki kitatafuta ishara lakini hakitapata kwasababu ya movu yao katika maandiko kadhhaa πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mathayo 16:4 "Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake."
Mathayo 12:38-39. "Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona."

Sasa ukitaka kuelewa vizuri unaweza ukarudi nyuma ukaona namna Gideoni alivyokuwa anashangaa kwamba walisimuliwa matendo makuu ya Mungu lakini kipindi chao hakuona yale matendo makuu ya Mungu ila ameona namna ambavyo taifa la Israel likiwa liko chini ya kongwa la utumwa wa wamidiani mpakka akawa anajiuliza wewe Mungu ikoje hapa lakini hakuwa amezingiatia kuwa taifa la Israel lilikuwa limeingia katika dhambi ndicho kitu kikawafanya wasiyaone matendo makuu ya Mungu.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Waamuzi 6:1,13 "Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA; BWANA akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani."

(Unaweza ukasoma pia waamuzi 2:10-15)
Kwahiyo mlango mkuu wa kanisa kutokuona matendo makuu ya Mungu ni kuto kujitoa kikamilifu kwa Yesu mwenyewe maana yeye ndiye mwenye matendo makuu, lazima tukubali kumfuata na kuacha yote kwaajili ya Yesu kristo Yesu.

C. KUPOTEA KWA KIBALI NA HESHIMA MBELE ZA MUNGU.

Mungu anapo liona kanisa lake likiwa limepoteza mwelekeo anaoutaka kwa kutokujitoa kwake mbele zake huwa anacho kifanya anaondoa mambo makuu mawili ambayo ni muhimu sana ambayo ni
A. Heshima
B. Kibali

Ufunuo wa Yohana 2:5 "Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu."
Ukisoma hapo juu unaona Yesu anazungumza kupitia kinywa cha Yohana kuwa lazima ukumbuke ulipoanguka ili utubu na usipofanya hivyo anakuja kuondoa kinara (Kibali na heshima) ambayo alikuwa amekupatia ili ubaki wewe mwenyewe maana haujafuata njia zake. Kama alivyokuwa ametaka. Hii kitu ndiyo ilimfanya pia hata petro kusema hiki kituπŸ‘‡πŸ‘‡

1 Petro 5:6 "Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;"

Kifupi ni kuwa kama ukinyenyekea (Umejitoa kikamilifu mbele za Mungu) yeye atakuinua kwa wakati wake( Yani atakupa Heshima). Kiufupi kama usipofanya hivyo uwe na uhakika atakupa aibu kabisa kwakuwa mkono wake hautakuwa juu yako na shetani atakuwa na uhalali wa kufanya kile anachokitaka kwenye maisha yako ya kila siku.

Naomba tuangalie japo kwa kifupi juu ya kibali ili kuweza kuelewa uzuri wa kuwa nacho kutoka kwa Mungu.
KIBALI
Mithali 8:35-36 "Maana yeye anionaye mimi aona uzima, naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, nao wanichukiao hupenda mauti."

Mambo muhimu kuhusu kibali
• Hii ni hali ya kupokelewa au kukubaliwa kufanya jambo au kupewa ruhusa ambayo sio watu wote wanapewa bali ni kwa wale waliochaguliwa tu.
• Pia, Kibali humaanisha kuonyeshwa wema, Yani Mungu anakutendea mema ambayo hata wengine huwa wanatamani kama wangeyapata lakini wameyakosa kwasababu ya namna Mungu ametaka mwenyewe.
• Pia hii ni hali ya kupewa upendeleo na Mungu
Mithali 12:2 "Mtu mwema atapata upendeleo kwa BWANA; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye"

Lazima uelewe kuwa kibali huwa kinatafutwa na huwa kinatunzwa kwahiyo kwa kujitoa kwako kikamilifu mbele zako mbele za Mungu kutakufanya upate hicho kibali cha Mungu lakini kama hautafuata matakwa yake utakipoteza kabisa.

MAMBO YA KUKUSAIDIA KUTUNZA KIBALI CHAKO KWA MUNGU
A. Jifunze kuwa na nia safi kabisa ndani yako kila inapoitwa leo
Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye."
1 Wakorintho 10:31 "Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. "

B. Jitahidi kufanya Mema mbele za Mungu
Mwanzo 4:5-7 "bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde."

C.Okoka kwa kumaanisha kwelikweli
D. Kuwa mtu wa Ibada.
Matendo ya Mitume 16:25-26 "Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa."


6. MAMBO YA KUFANYA ILI KULISAIDIA KANISA KUMAANISHA KUJITOA KWAKE.
Mungu wetu ni mwaminifu sana ambaye ametupa maarifa ya kuweza kutusaidia kumaanisha kujitoa kwetu. Kwahiyo kuna baadhi ya mambo ambayo yanaweza kutusaidia kumaanisha kujitoa kwetu kwa Mungu wetu. Mambo yenyewe ni kama ifuatavyo
A. Kumjua Mungu
B.kuwa rafiki wa Neno la Mungu
C. Kumpenda Mungu na mambo yake yote
D. Kuchagua uaminifu na utii
E. Kuwa mtu wa Ibada, Maombi na kutenga muda wa maana na Mungu wako.

A. KUMJUA MUNGU
Moja ya jambo la kumsaidia mwamini kuweza kumaanisha kujitoa kwake ni kumjua Mungu vizuri ili kwamba kwenye kuamua kwake kujitoa anaelewa kwanini ameamua kuambatana naye. Kiufupi nguvu ya kujua inauwezo ndani yake wa kuambatanisha. Huwezi kuambatana na mtu usiye mjua wala huwezi kumuamini kwahiyo ukimjua Mungu utaambatana naye na utamuamini kwakuwa unaelewa kila kitu chake.

Ayubu 22:21 "Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia."

Mtu anapomjua Mungu huwa amani kwake sio kitu cha kuuliza wala kufikiria maana wakati wote anakuwa ana uelewa wa nini anakifanya. Kwahiyo hata kama akiamua kuambatana na Mungu hata yakija magumu hayawezi kumtoa kwenye msitari wa kuendelea kuambatana na Mungu wake na ndio maana Daudi anasema πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Zaburi 119:165 "Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza."

Sasa ukimuangalia mtumishi wa Mungu paulo anaeleza namna ambavyo amejitoa kwa kristo Yesu na kuyaona mengine yote kuwa kama mavi, lakini anatamani kumfahamu Mungu wake vizuri kwa kutokutumia haki yake mwenyewe bali kwa imani ipatikanayo katika kristo Yesu kitu kitakachomfanya aweze kumshika Mungu wa mbinguni kiukwelikweli na kuweza kuambatana naye siku zote.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Wafilipi 3:9-10 "tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;"

B. URAFIKI WA KWELI NA NENO LA MUNGU
Neno La Mungu huwa linatoa mwongozo wa namna ya kuishi katika maisha ya kila siku. Mtu anapokuwa rafiki wa Neno la Mungu kila hatua atakayokuwa anaiamua Neno litampa mwongozo na kumfanya aweze kuamua kikamilifu kujitoa kwaajili ya Yesu kristo.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Zaburi 119:105 "Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu."

Mungu ndiye pumnzi na uhai wetu na ndio maana hata kipindi cha Yoshua alimsisitiza kuishika sheria yake kila wakati ili kupitia hiyo imuongoze kwenye maamuzi kwakuwa toka asili Neno la Mungu ndio msingi wa ki maongozi kwa mtu yeyote ambaye amekubali kumfuata MunguπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Yoshua 1:8 "Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana."

Mungu siku zote anachokitaka kwa kanisa lake ni ule moyo wa kuwa tayari kusikiliza Maneno yake na kuyatenda na kuhakikisha tunaishi katika hayo. Katika Neno ya Mungu tunapata kuwa salama na ndio maana hata Suleiman alipokuwa ameandika mithali kuna sehemu alisema hiviπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mithali 4:20-22 "Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako;
Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote."

Ukijiuliza ni kwanini mtumishi wa Mungu huyu alisema jambo kama hili unagundua kwamba alikuwa akitamani watu wasikilize mahusia ya Mungu (Neno La Mungu) ambalo hilo unakuwa unamzungumzia Yesu kristo mwenyewe (Yohana 1:1-5) ambapo anatamani tumshike yeye yaani tujitoe kikamlifu kwaajili ya Mungu wetu maana katika yeye tutakuwa hai ikiwa tutamkimbilia. Unaweza ona namna ambavyo hata paulo alisema na watu wa Athene alipowakuta wakiabudu kwa Mungu asiyejulikana na akawatambulisha Mungu anayejulikana na kuwaambia kuwaπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Matendo ya Mitume 17:28 "Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.

Ikiwa Uhai unapatikana kupitia Yesu kristo kwahiyo lazima tuwe na urafiki na Neno la Mungu ndipo tutaweza kujikuta tumeweza kulishika Neno La Mungu kikamilifu kabisa na kujikana kwaajili ya kristo Yesu. Jambo lingine mambo mengi tunayaweza kwasababu tumekaa ndani ya Yesu kikamilifu kwahiyo nguvu ya uwezesho wa kujitoa na kujikana kwetu huwa mara nyingi tunapewa kama zawadi tu na Mungu mwenyewe kupitia Kristo Yesu. Ndio maana hata Yesu alizungumza na wanafunzi juu ya kukaa ndani yake ili waweze kuzaa matunda yani kiufupi uwezo wako wa kujikana kikamilifu kwaajili ya kristo Yesu unatokana na Yesu mwenyewe (Urafiki wa kweli na Neno la Mungu).πŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 15:5-6 "Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea"


C. KUMPENDA MUNGU NA MAMBO YAKE YOTE.
Mambo mengi huwa tunaweza kuyafanya ni kwasababu Mungu ametuwezesha lasivyo vitu vingi tungeshindwa kuvifanya (Wafilipi 4:13, 2timotheo 4:17). Sasa kwasababu mambo yote tunawezeshwa na yeye ni jambo moja Mungu analolitafuta kwetu ambalo kila wakati aangetamani tuweze kuishi katika njia hiyo ambayo ni Upendo na ndio maana katika kuzitaja amri yeye alitupatia amri moja kuu inayobeba kila kitu ambayo ni upendo.

Mathayo 22:36-40 "Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii."
.
Nimekuambia kuwa unapaswa kumpenda Mungu na mambo yake yote kwasababu kupitia Upendo ndipo utaweza kufanya maamuzi yaliyo sahihi ya kuamua kuambatana na Mungu kwenye maisha yako na kujikataa mwenyewe kabisa, hii ndio sababu hata ukiingia kusoma agano jipya ndipo unaona msisitizo wa mitume ulikuwa juu ya kufanya vitu kwa upendo mfano kwa habati ya utoaji (2wakorintho 9:7). Pia pale utakapo kuwa umempenda Mungu hata kama utapitia magumu hautakata tamaa kumuishia Mungu utajikuta kila kitu kwako ni amani maana yupo Mungu akupaye amani.

Zaburi 119:165 "Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza."



D. CHAGUA UAMINIFU NA UTII
Uaminifu ni hali ya kitabia ambapo mtu anachagua kusimama katika makubaliano, ahadi, wajibu na mahusiano pasina kuangalia upande wa pili hata kama yale mambo yanamuumiza.
Wakati
Utii ni kitendo cha kusikiliza, kukubali na kutenda kulingana na maagizo, sheria au mapenzi ya mamlaka halali, kwa hiari na heshima.

Sasa haya mambo mawili yaani uamini na utii lazima ukubali kuambatana navyo maana katika hivyo Ndipo kuna ufunguo wa kubaki katika mshikamano. Kuna wakati lazima wewe uweke dhamira ya ndani ya kutaka kujikataa kwaajili ya Kristo Yesu ili Mungu aweze kukupa hiyo neema ya kuweza kujidhabihu kweli kweli na ndio maana samweli alimwambia sauli kuwaπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

1 Samweli 15:22-23 "Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme."

E. IBADA, MAOMBI NA MUDA WA MAANA NA MUNGU.
Maana Ya Ibada
Neno Ibada linaweza kutafsirika kwa namna mbili ukitumia maneno ya kigiriki cha biblia(Kiyunani) ambayo ni "Proskuneo" na neno "Latreia"

"Latreia": humaanisha Huduma ya ibada, kumtumikia Mungu ambpo sasa Huhusisha maisha ya kujitoa kwa Mungu, si matendo ya nje tu bali mpaka utu wako wa ndani kabisa.πŸ‘‡πŸ‘‡

Warumi 12:1 "Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana."

"Proskuneo": humaanisha Kusujudu, kuinama kwa heshima na unyenyekevu. Hii Inaonyesha mtazamo wa moyo na mwili mbele za Mungu.πŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 4:24 "Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli."

Pale kanisa/mwamini anapochagua kuwa chombo cha ibada huwa wakati wote Mungu anakuwa anafanya kazi pamoja naye, kitu kitakachomsaidia yeye mwenyewe kuendelea kujitoa kwa Mungu wake aliye muita na kumuokoa. Ibada siku zote inakuwa inaambatana na Maombi ambapo lazima utafute mda mzuri wa kuzungumza na Mungu wako ili akupe maelekezo ya namana ya kuishi kitu kitakachokusaidia kuwa salama na kujitoa kikamilifu mbele zake. 
Jambo ambalo lilimfanya Yesu aweze kujitoa kikamilifu mbele za Mungu ni ule utayari wake aliokuwa anamfanyia Mungu ibada, pia alikuwa ni mtu wa maombi na alitafuta muda wa maana usiokuwa na vurugu za aina yeyote ambapo na sisi tunapaswa kufuata msingi huo lasivyo tutapotea pasina kujua.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Marko 1:35 "Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko."

Luka 22:39 "Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye."

Mungu akubariki kwa kuambatana nami katika mfululizo wote wa tatu katika somo hili Mungu aliliweka ndani yangu

Kama una swali au sehemu hujaelewa unaweza ukawasiliana nami kupitia mawasiliano hapo chini.

Ulikuwa nami mtumishi katika kristo Yesu
Jina: Bro Jackobo
Number: +255766944441
Email: jackobombwaga@gmail.com

KUJIKANA NDANI YA KRISTO YESU (sehemu ya pili)


Bro Jackobo

Utakuwa nami mpendwa katika kristo yesu
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com


Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu?? Karibu Tena kwenye sehemu hii ya pili ambapo ni muendelezo wa somo la Kujikana ndani ya Kristo Yesu ambapo tuliona maana ya kujikana ndani ya Yesu kristo, Tuliona nani alikuwa mwanzilishi wa kujikana tangu asili ambaye ni mfano wetu wa kuigwa tukamalizia na maeneo muhimu mawili ambayo mwamini anapaswa kuonyesha na kuthibitisha kuwa amejikana ndani ya kristo Yesu. Kama hujalisoma somo hilo naomba uende usome sehemu ya kwanza kwa kubonyeza hapa SEHEMU YA KWANZA.
Leo tutaanzia kwenye kipengele cha vipingamizi katika kujikana ndani ya Kristo Yesu.

4. VIPINGAMIZI KATIKA KUJIKANA KWA MWAMINI NDANI YA KRISTO YESU.
Tunapozungumza juu ya Vipingamizi tunaangalia juu ya mambo au vitu ambavyo vinaweza kuleta shida kwa mtu huyu ambaye anataka kujitoa kwa ajili ya kristo vinakuwa vinamrudisha nyuma licha ya yeye kutaka kusonga mbele kwenye kujitoa kwaajili ya Yesu wake aliye muaamini. Watu wamejikuta wanakumbana na vikwazo vingi sana vinavyowafanya washindwe kujidhabihu vizuri katika eneo la utumishi na Utakatifu na utaua.

Vikwazo hivyo ni kama ifuatavyo
A). Upinzani wa ndani ya nyumba ya Mungu/kanisa
B). Upinzani wa nje ya nyumba ya Mungu/kanisa
C). Fedha
D). Msimamo wa kiuaminifu katika mahusiano baina ya jinsia mbili
E). Vyakula
F). Uelewa mdogo wa Mungu unayemuabudu
G). Vyeo vya kiuongozi

A. UPINZANI WA NDANI YA NYUMBA YA MUNGU/KANISA
Hivi vizuizi vinakuwa vinatokana na mazingira ya ndani kwenye nyumba ya Mungu ambayo yanamfanya huyu mtumishi wa Mungu ashindwe kuishi ule utayari wake wa kumtumikia Mungu ambapo ndio kujikana halisi kwa mwamini.

Mathayo 16:21-23
"Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu."

Ukiangalia hapo juu utaona Yesu alikuwa akikemewa na petro kwamba hata pitia mateso lakini Yesu hakumsikiliza Petro bali aliangalia mbele ili kutimiza kusudi lake lililomleta. Tulitegemea kwamba Petro asiwe kikwazo au kumvunja moyo Yesu kutimiza kusudi japo kwa akili ya kibinadamu ilikuwa ni ngumu sana kuelewa ule utumishi ambao ilitakiwa Yesu kuupitia. Hii ndio inatufanya hata nasi kama waamini lazima tuelewe vizuri ni kwa namna gani Mungu ametuita ili tuweze kumtumikia na kama tusipoelewa ndio tunajikuta sasa tunaishia kuvunjwa moyo na watu watu wa karibu au ndani ya nyumba ya Mungu.

Unaweza ukavunjwa moyo na watumishi wa Mungu mfano Mwalimu, mchungaji, mzee n.k lakini usiache kufanya kazi ya Mungu. Wewe hakikisha unamtazama kristo tu kama kielelezo chako katika kumtumikia Yeye.

Kwa namna gani upinzani wa ndani unaweza kuwafanya waamini wakate tamaa??
1. Kuzuiliwa katika huduma na kiongozi wako wa kiroho; usiaangalie ni kwa namna gani kiongozi wako kakuambia au kukukataza kutumika kikubwa jihakikishe uhusiano wako na Mungu halafu uendelee kumuomba Mungu ili akupe namna ya kutumika.
2. Maisha ya dhambi kwa viongozi wa kiroho wanaosimama mbele ya madhabahu; watu wengi wanaosimama mbele ya madhabahu wamekuwa wakiwavunja moyo watumishi wengine kutumika kwa kuwa na maisha mabovu sana. Japo usimfanye mwanadamu akawa ni kielelezo chako kwenye kumtumikia Mungu maana wanadamu watakukatisha tamaa lakini wewe mtazame Yesu na umfuate na sio vinginevyo.
NOTE: HUU UPINZANI WENGI UNAWAINGIZA KWENYE MTEGO KWASABABU YA KUTO KUMUELEWA MUNGU WANAYEMTUMIKIA PAMOJA NA KUSUDI WALILOLIBEBA NDANI YAO.

B). UPINZANI WA NJE YA NYUMBA YA MUNGU/KANISA (WATU WASIO AMINI)
Hapo mwanzoni tumeona upinzani unaopatikana ndani ya nyumba ya Mungu na kumfanya huyu mtu akashindwa kujikana kwaajili ya kristo Yesu, lakini hapa tutaona mambo yanayoweza toka nje ya ya nyumba ya Mungu (wasio Waamini) na kumfanya huyu mtu akarudi nyuma.

Yohana 16:1-3
"Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi."

Yesu aliamua kuwaambia wanafunzi wake juu ya changamoto na upinzani watakao upata kutoka kwa watu wa dini ya kiyaudi ili kwamba wasije vunjika moyo hata siku moja. Na aliwaambia hivyo maana alijua wapo watakao fanya kama kuwaua kabisa wakijua ya kwamba wanamtumikia Mungu lakini kiuhalisia hawako kumtumikia Mungu bali wanafanya kazi ya shetani.
Pale ambapo ukikutana na watu wanakupiga vita juu ya kumtumikia Mungu huko nje usije ukaacha kumtumikia Mungu hata siku moja wewe fanya kazi ya Mungu tu hata kama mazingira ni magumu sana.
Kuna watu huwa wanakataliwa na ndugu na kutengwa na familia kabisa kisa wamemkubali Yesu, sasa hata kama yakikutokea hayo jua tu kuwa ni upinzani wa nje unaotaka kukukwamisha usimuishie Mungu wako uliyekubali kujikataa kwaajili yake, Fanyauwezavyo usiingie katika huu mtego utakuwa salama sana yani.

Note: Watu wamekuwa na urafiki usiokuwa na mipaka kiasi kwamba hawawezi tena hata kuwaambia watu wengine juu ya utumishi wao walio nao. Kwahiyo watu wako wa nje na nyumba ya Mungu lazima uishi nao kwa kwa akili sana ili usije ukapoteza lengo la kuishi. Hakikisha maisha yako mwenyewe ni ushuhuda tosha kwa ajili ya kukurahisisha kuweza kuwahudumia wale walioko nje waujilie ule upendo wa Kristo Yesu.

C. FEDHA
Fedha na dhahabu vyote hivi ni mali ya Mungu mwenyewe (Hagai 2:8) hivi vyote Mungu amempa mwanadamu awe ni wakili juu yake kwahiyo hata kwenye matumizi yake yanahitaji neema ya Mungu sana ili mtu asitoke katika msingi wa Neno lake. Sasa katika kanisa letu la leo tumehama kabisa kutoka kwenye uwakili wa hizo mali tumepewa na Mungu kiasi kwamba tumechagua kuiweka mioyo yetu kwenye mali zetu kwa kuzipa kipaumbele kuliko hata kumpa Mungu nafasi ya kutuongoza.  Hapa tunapewa maonyo na mtumishi wa Mungu juu ya fedha.

1 Timotheo 6:10 "Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi"

2 Timotheo 3:1-2 "Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi"

Sasa ukisoma hapo unaona ya kwamba kuwa na pesa sio kitu kibaya ila kuuhamishia moyo wako kwenye pesa na kuzipenda kunakuwa ni mzizi wa mambo mengi mabaya kuweza kutokea maana ukiwa katika hali hiyo unaweza kufanya jambo lolote pasipo hata kufikilia mara mbili juu ya madhara yanayoweza kutokea kwa maamuzi yako.

Ukiwa mtu wa kupenda sana fedha ni ngumu sana kumuabudu Bwana na ndio maana hata maandiko yanatuonyesha kuwepo kwa mabwana wawili ambao ni Fedha na Mungu ambapo haiwezekani ukavitumikia vyote kwahiyo lazima uchague kimoja cha kwenda nacho ndipo utakuwa salama.

Mathayo 6:24 "Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali."

Hii inatuonyesha namna pesa ilivyo na nguvu sana ya kuteka mioyo ya watu kama hawataangalia na kukaa vizuri kwenye nafasi zao. Kwasababu ya fedha kuwa na nguvu ya kushika mioyo ya watu, watu wengi wametupilia mbali ule ujasiri wao na kujikana kwao kwaajili ya kristo Yesu wameanza kutafuta tu pesa. Watu wengi wameacha mambo ya ki Mungu kabisa mfano Kuhubiri injili, kuwepo kwenye makusanyiko ya ki imani wako busy na mambo ya kutafuta fedha na ndio maana ukienda makanisani siku za jumapili utakuta watu wengi sana lakini siku za katikati huwezi kuwakuta watu kwasababu wengi wao wako busy kutafuta pesa wameacha nafasi ya Mungu na hata ndani ya mioyo yao hawajihisi hata Hatia au kukosea kwakuwa fedha zimekuwa Bwana kwao. Mungu atusaidie sana kwenye eneo hili tusije kutekwa mazima tukapotea

NAMNA GANI FEDHA IMEKUWA KIKWAZO KWA WATU KWENYE KUJIKANA KWAAJILI YA KRISTO YESU?? 
1. Watumishi kuwashikilia watu wenye Fedha kwenye uongozi ingali wanafanya maovu; Hii imekuwa kikwazo sana maana wachungaji wengine wamejikuta wakilitukanisha jina la Mungu kwasababu hiyo maana wanakuwa wameyachagua matumbo yao badala ya kumchagua Mungu wa ibada za kweli.

2. Watu wanadanganya ili wapate fedha: Kitendo cha kukubali kudanganya na kupata fedha ni dhahiri kabisa kuwa umeuacha upendo wa Mungu na kuushika mwenendo usiokuonyesha kujitoa kwako kwa Mungu. Mfano Gehazi alikubali kudanganya ili apate fedha (2wafalme5:21-23).

3. Kuanguka kwenye zinaa (Uasherati na uzinzi) ili kupata fedha: Dunia ya leo imejaa Zinaa sana kiasi kila utakapopita kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali masuala ya ngono yanapewa matangazo makubwa sana kiasi kinawafanya wengi kuanguka kwenye mtego kirahisi lakini wengine wanaingia huko ili wapate fedha ambapo ni jambo la kutisha sana tena sana.

4. Watumishi wengine wanatumia nguvu za giza kwenye huduma zao ili wapate washirika wengi lengo ikiwa ni kupata fedha kutoka kwao:

Wito wangu naomba usikubali fedha ikakutoa kwenye mpango wa Mungu aliokuitia hakikisha unaupa ufalme wa Mungu kipaumbele kwanza kabla ya hizo mali na uchumi unao utafuta na Mungu katika hayo atakuzidishia sana tena sana.


D. MAHUSIANO BAINA YA JINSIA MBILI TOFAUTI
Moja ya maeneo yamekuwa ni changamoto sana kwenye kizazi cha leo ambacho Mungu mwenyewe alikiita kizazi cha zinaa (Mathayo 12:36, 16:4) ni kuwa na uaminifu kwenye uhusiano wanao kuwa nao baina ya jinsi mbili yani mwanamke na mwanaume. Watu wengi wako makanisani lakini uasherati na uzinzi ni kitu cha kawaida sana kwao na wala hata hawaogopi kabisa wanaona tu ni kawaida yani wameizoelea neema ya Mungu kiasi kwamba hata wanapoonywa hawawezi kumtii Roho wa Mungu.

Mungu anataka watu wasiingie kwenye huu mtego wa zinaa kwa namna yeyote lazima wayajue mapenzi ya Mungu ndipo wataweza kushinda lasivyo wataanguka kwa mtego wa adui na ndio maana Suleiman anaseme kwenye Mithali mambo haya hapa

Mithali 6:25-26 "Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate;
Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani"

Mithali 5:15-20 (15-16) "Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako. Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali, Na mito ya maji katika njia kuu? 

Baada ya Mungu kusema na vijana wasio na ndoa na kuwaonya juu ya kuwa na uaminifu kwenye eneo hili anasema pia juu ya wanandoa kubaki kwenye kiapo chao na kuwa waaminifu kwa kutokutoka nje ya ndoa zao (Kunywa maji ya birika lako mwenyewe) hii itakufanya kuwa mtu ambaye umejikana kikamilifu sana mbele za Mungu wako lakini isipokuwa hivyo utakuwa wewe haujajikana mbele za Mungu hata kama unaingia nyumbani mwa Mungu".

Unaweza ukasoma maandiko haya kwa faida yako zaidi (1WAKORINTHO 6:9, WAGALATIA 6:7-8).



E. VYAKULA
Watu wanaweza wakashangaa kwa namna gani chakula kinaweza kikamfanya mtu akashibdwa kujikana vizuri mbele za Mungu!! Ila naomba fuatana nami, watu wengi huwa wanajikwaa sana katika eneo la chakula mfano akikosa chakula yuko tayari kumuacha Mungu wake ili alishibishe tumbo lake, wengine wametoa hata rushwa ili wapate chakula chao cha kila siku, wengine walifika wakamnung'unikia Mungu kwasababu ya kukosa chakula

Kutoka 16:2-3 "Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote."

Wana wa Israeli walikuwa wanafikiria chakula walichokiacha misri na kuacha kumtazama Mungu mpaka wakawa wanamlaumu Mungu kwanini aliwatoa misri wakasahau mateso waliyokuwa wanayapata mpaka wakawa wanamlilia Mungu. Kwahiyo kukosa chakula kusikufanye ukamkosea Mungu au ukamtukana Mungu wako hata siku moja bali chagua kumuheshimu Mungu wako.

Tumekuwa na masherehe mbalimbali kwenye kizazi chetu lazima uchague kumtukuza Mungu tu kwenye eneo hili, wengine wameingia kwenye mtego wa kushiriki hata vyakyula vilivyotolewa kwa sanamu/ vyakyula ambavyo vinaleta machukizo mbele za Mungu mfano Pombe n.k. lazima tujifunze kwa mtumishi wa Mungu Danieli namna alivyo azimia moyoni mwake na akapata kibali na kumtukuza Mungu wake kupitia hiloπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Danieli 1:8 "Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi."

F. UELEWA MDOGO WA MUNGU WAKO UNAYEMUABUDU
Moja ya msingi mkubwa wa upotovu kwa maisha ya mwamini ni uelewa mdogo juu ya Mungu wako, haiwezekani kujitoa kikamilifu hata siku moja kwa Mungu usiyemjua kikamilifu lasivyo utakuwa unapapasapapasa tu kitu kitakacho kupoteza kwenye ramani ya ki Mungu.

Kutoka 32:1-6(1)
Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.

Wana wa Israel walikuwa hawamjui Mungu wao ambaye amewatoa nchi ya utumwa bali walimjua Mussa na ndio maana baada ya Mussa kuchelewa waliamua kuchonga sanamu kitu kilicho mchukiza sana Mungu kwakuwa hawakumpa heshima aliyokuwa amestahili. Watu wengi hawamfahamu vizuri Mungu wanaye Muabudu na ndio maana wanaweza kufanya mambo ya ajabu ajabu tu mbele zake na wengi wapo kwa nyumba ya Mungu lakini hawawezi kujitoa kikamilifu mbele zake.

G. VYEO VYA KIUONGOZI
Kanisa Tulilo nalo kwasasa limekuwa na changamoto sana kwenye eneo hili yani wachungaji wamekuwa wakifanyiana hata mambo ya ajabu, washirika wamekuwa wanachafuana lengo ni kuweza kupata nafasi za kiuongozi kitu ambacho kimewapelekea wengine kutenda dhambi kitu kinachowafanya wawe hawajajitoa kikamilifu mbele za Mungu kama ambavyo anataka Mungu wetu.
Herode alitaka kumuua Yesu kwasababu ya kuhofia kupoteza nafasi yake ya kiuongozi kitu kilicho mfanya akaamua kuangamiza watoto wote chini ya miaka miwili (MATHAYO2:1-18). Jambo kama hili halifai kuonekana kabisa kwa mtu ambaye amekubali kumuamini Yesu kristo kwahiyo jifunze kuondoa wivu utakuwa salama. Ona hapa namna sauli pia alivyoharibikiwa.

1 Samweli 18:6-9 "Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile."

Ukisoma utaona namna Sauli alivyojaa wivu kwasababu ya kuutaka uongozi kiasi alikuwa tayari kumuua Daudi ili asiwe na mpinzani wa aina yeyote kwenye nafasi ya ufalme, Ndugu yangu usije ukaingia kwenye mtego wa kutaka kuwa kiongozi na ukamtukanisha Mungu wako kwakufanya mambo ya ajabu, Rizika na mahali Mungu amekuweka ukae na cheo alichokupa ili jina la Mungu litukuzwe na akuinue kwa wakati wake anaoona kwake unafaa kwako.


Mungu akubariki kwakuwa nami Sehemu hii ya pili ya mfululizo huu. Wa Somo letu hili Zuri, naomba usiache kufuatilia muendelezo wa sehemu ya tatu na ya mwisho kwenye somo letu hili, naamini utapata kitu cha kukupa hatua ya kiroho zaidi

Ulikuwa nami mpendwa na mtumishi katika kristo Yesu
Jina: Bro Jackobo
Namba: +255766944441
Email: Jackobombwaga@gmail.com
Blog: jackobombwaga.blogspot.com

KUJIKANA NDANI YA KRISTO YESU (Sehemu ya kwanza)


Bro Jackobo


Utakuwa nami mpendwa katika kristo yesu
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com

UTANGULIZI
Katika kizazi hiki cha Utandawazi (Sayansi na teknolojia) Tumekuwa na kanisa ambalo limekuwa likienda pasina utaratibu huku likijiona kukamilika sana kuliko hata Yesu kristo mwenyewe. Watu wamekuwepo nyumbani mwa Mungu lakini Dhambi kwao ni kitu cha kawaida wala hawana hata Hofu kidogo na wanajiona ya kuwa wako katika msitari wa Mungu huku wakipuuza maagizo yake. Mungu anatafuta moyo wa mtu ambaye amekubali kuacha mambo yote kwaajili yake na ndio maana Mungu kanipa kuleta hili Somo "Kujikana Ndani ya kristo Yesu" liweze kutusaidia ili tubaki katika msingi wa Ki Mungu ambao yeye ameukusudia tuweze kuishi katika huo.

Somo letu limegawanyika katika maeneo makuu sita yanayomfanya huyu mtu aweze kujikana kikamilifu ndani ya kristo Yesu. Karibu tuambatane kwa pamoja ili tuweze kuelewa kiundani zaidi.

Maeneo Muhimu ya somo Letu.
1. Maana ya Kujikana Ndani ya Yesu kristo
2. Mwanzilishi /Mwasisi wa Kujikana
3. Maeneo Muhimu mwamini anapaswa kujikana
4. Vipingamizi kwa kanisa katika kujikana kwa Kristo Yesu
5. Madhara yanayoweza kutokea kwa kanisa kushindwa kujikana Mbele za Yesu Kristo
6. Mambo ya kumsaidia Mwamini kumaanisha kujikana kwake.




1. MAANA YA KUJIKANA NDANI YA YESU KRISTO
Neema ya Mungu imefunuliwa kwetu kiasi kwamba inatuelekeza Yenyewe namna ya kupata maarifa sahihi katika neno lake na ndio maana anasema Yeye ni Mungu ambaye huwa anatufundisha tuweze kupata faida πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Isaya 48:17 "BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata."

Sasa ni nini maana ya kujikana ndani ya Yesu kristo? Tunamaanisha nini tunaposema huyu mtu amejikana kwaajili ya Yesu kristo? Je kila ambaye ameokoka amekwisha kujikana ndani ya kristo Yesu? Je ipo siri gani tunayotakiwa kuishika au kuiishi ili tuwe tumejikana ndani ya Yesu kristo?

Kujikana ndani ya Yesu kristo ni hali ya kuacha mambo yako yaliyokuwa na heshima, ufahari na kukupatia faida kwa ajili ya kufanya mapenzi na makusudi ya Mungu kupitia kristo Yesu.

Kwa mwamini Yeyote yule ni lazima mambo yote anayoyafanya yapitie kwa kristo Yesu ili aweze kupata uhalali na haki yaani kifupi haki ya mwamini yeyote mbele za Mungu ipo ni kwasababu Yesu kristo amesimama na ndio maana kuyafanya mapenzi ya Mungu ni lazima tupitie kwa Yesu kristo kwakuwa Yeye ndiye njia ya kweli na uzima na hakuna anayeweza kumwona Mungu bila yeyeπŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 14:6 ,"Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi."

Sasa kuna andiko la msingi hapa linalobeba Somo letu la siku ya Leo ambalo ndio funguo la yote tutakayojifunza kwenye huu Mfululizo wa somo hiliπŸ‘‡πŸ‘‡

Luka 9:23-24 "Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha."

Ukiangalia hapo Yesu alipokuwa akisema na wanafunzi wake alikuwa anawaandaa katika hali ya kumuishia Mungu katika mantiki ya kwamba wayahesabu mambo yao sio ya maana bali waone kwamba mambo ya Kristo Yesu ndio ya maana zaidi. Hii ilimfanya ifike wakati sasa awaambie wajikatae/kujikana ili kwamba wamfuate Yesu na huku wamebeba mizigo/msalaba/mateso yao. Mungu alikuwa anawafundisha namna ya kutoa kipaumbele mambo yote yanayomhusu Mungu na sio yazifurahishazo nafsi zao hata kidogo. Hapa pia alikuwa akiwaonyesha kwamba katika kristo sio kwamba watapata kufurahi tu bali hata mateso yangewakuta kwaajili yake.

Mtu anapoamua kujikana kwa ajili ya Yesu kuna kuwa na tabia au mwenendo ambao anapaswa kuuacha na kuambatana na mwenendo au tabia atakayoambiwa baada ya kukubali wito wake. Kuacha tabia zako ulizokuwa nazo sio kitu rahisi hata kidogo kwasababu ya uraibu unaokuwa umejijenga kwa hizo tabia. Mfano kwa vijana ambao huwa wanajichua au wanafanya Punyeto (masterbation) huwa sio rahisi sana kuacha kwasababu kuna kumbukumbu linalo waendesha ndani yao litokanalo na kemikali ndani ya mwili iitwayo Dopamine inayomsukuma kurudia ili aweze kupata ile furaha (pleasure) aliyowahi kuipata. Kwahiyo ili aweze kuacha lazima kuwe na nguvu ya kumsaidia huyu mtu ambayo imefungwa ndani ya kristo ambapo anataka sasa tuende na mizigo (tabia) Yetu ili aweze kutupumnzisha (kutuondolea).πŸ‘‡πŸ‘‡

Mathayo 11:28-30 "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi."



2. MWANZILISHI/MWASISI WA KUJIKANA.
Nani alikuwa mwanzilishi wa kujikana??
Note: Mwanzilishi mkuuu wa kujikana alikuwa ni Yesu mwenyewe kwa namna ambavyo aliacha Enzi na utukufu wake akaja kutuokoa sisi. Na aliona kwamba ile heshima na utukufu wa ki-Mungu sio kitu cha maana ila kukamilisha ule wito au kule kukubali kwake kujitoa kwa ajili ya maisha yetu hata ukafika hatua akawa yuko tayari kunyenyekea hata mauti ili aweze kutupata sisi ambao tulikuwa tumepotea.

Wafilipi 2:5-7
"Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;"


Pia Yesu aliweza kutuchagua sisi licha ya kwamba tulikuwa na dhambi ili kwamba atufanye sisi tuwe wana wa Pendo lake na sio sisi tuliomchagua yeye. Sasa huku kwa yeye kutuchagua kunaonyesha kujikana kwake mbele ya Mungu baba ambako pia ndio mfano tunatakiwa kuufuata.

Yohana 15:16
"Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni."

Katika kujitoa/kujikana kwa Yesu kristo ndiko ambako mwamini inatakiwa afuate mfano wake na sio mfano wa mwanadamu awaye yeyote. Hii ilimfanya mpaka atupe uhakika wa kuweza kufanya mambo ambayo ameyafanya na zaidi ya yale aliyokuwa ameyafanya. Ona hapa ambapo alituthibitishia ili kwamba tukiwa na hekima na maarifa ya Ki-Mungu tuweze kufuata njia yakeπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 14:12
"Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba."

3. MAENEO MUHIMU AMBAYO MWAMINI ANATAKIWA KUJIKANA NDANI YA KRISTO
A. Utumishi
B. Maisha ya utakatifu na utauwa.

A. UTUMISHI
hii ni hali ya kuwa na utayari wa ndani wa kutekeleza majukumu/maagizo ambayo Bwana wako amekupa ili uweze kuyatekeleza.
Utumishi ambao Yesu ameuweka kwa mwamini ambaye amechagua kuwa na Yeye huwa umejikita sana katika maeneo haya
A. Kuitwa
B. Kutumwa
C. Utekelezaji

A). KUITWA: ili kuenda kutekeleza majukumu ya Mungu lazima akuite kutoka katika majukumu uliyo nayo na kuyaacha ili uyafanye mapenzi ya Mungu aliyekuita. Ukiwa kama mtu unayetaka kujikana kwa ajili ya Kristo Yesu usije ukaingia kwenye utumishi kisa umekosa kazi ya kufanya bali acha kazi yako ili uweze kumtumikia Mungu na ndio maana yeye alio waita waliacha walivyo navyo ili wamaanishe kule kuacha kwao πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mathayo 4:18-22 "Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata."

B. KUTUMWA: Watu wengi huwa wanasikia sauti ya Mungu ikiwaita kwenye utumishi lakini huwa wanakurupuka kwenda kutumika pasina kupokea maelekezo Mungu anayotaka wewe uyaishi katika eneo lako. Kwahiyo lazima ujifunze kuelewa sauti ya Mungu katika utumishi wako ili kujitoa kwako kwake kuwe na maana. Muone mtumishi wa Mussa alichokifanyaπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Kutoka 3:10-12
"Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu."

Ilikuwa inatosha tu kwa Musa kuondoka kwenda kuwatoa wana wa Israel lakini alitaka kupata taarifa kiundani zaidi ili hata kama akiulizwa kitu awe na majibu ya kuwapa. Usiende kufanya kazi ya Mungu pasina kuwa na maelekezo kamili ya Mungu aliye kuita maana ile kazi utaifanya sio kazi yako wewe bali ni ya yeye aliyekutuma kwenda kuifanya hiyo kazi ya Mungu.

C. UTEKELEZAJI: sasa hapa ndipo ambapo huyu mwamini anakamilisha kile kitu ambacho Mungu anataka akifanye. Lazima huyu mwamini akubali kufanya kazi ya Mungu haijalishi hali yake itakuwa inamuambia nini, hata kama unajiona huwezi lakini hapa lazima uyatekeleze yale ambayo Mungu amekupa kuyafanya na uyaache yale kwako unaona yana umuhimu ili jina la Bwana litukuzwe kupitia utumishi wako wa kila siku.

Wafilipi 3:7-8
"Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;"

Paulo kwa ajili ya kristo aliamua kupata hasara ili aweze kumpendeza kristo ambaye alimuita ili aweze kumtumikia yeye na huku ndiko kujikana ambapo Kristo alitamani wanafunzi wake wawe kama namna ambavyo paulo alikuwa tayari kuingia gharama/Hasara (Kuna gharama katika kumtumikia Mungu ambayo mwamini lazima akubali kuibeba). Paulo aliacha mshahara na marupurupu mbalimbali kutoka kwenye dini ya kiyahudi ili aweze kumpendeza Mungu.

Siku zote kama mwamini lazima ufike hatua na kuwa na utayari wa kuacha yote ili uweze kuitimiza ile kazi ambayo Mungu amekupa wewe kuifanya kama vile ambavyo paulo alifanya. Pia ukitaka kuelewa hata Petro ilibidi amuulize Yesu kwamba itakuwaje maana tumeacha yote nini kwako tutapata.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mathayo 19:27-29 "Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele."

Unapokubali sasa kujikana kwaajili ya ktisto ni lazima sasa ukubali kutii yale ambayo Yesu aliyasema. Ndio maana Yesu alipokuwa anaondoka aliwaambia wanafunzi juu ya utumishi katika kuieneza injili yake na sio vinginevyo. Na alitamani wanafunzi wake wawe hivyo onaπŸ‘‡πŸ‘‡

Marko 16:15
"Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe."

Sasa wewe uliye tayari kuwa na Mungu lazima ukubari kuihubiri injili kwa mazingira yawayo yoyote ili kuonyesha utayari wako kumtumikia Mungu katika eneo ambalo amekupa uweze kutumika.

Usikubali kukaa tu ndani ya nyumba ya Mungu pasina kuwa na kazi yeyote lazima uwe tayari kuifanya ile huduma ambayo Mungu amekupa wewe.


B. MAISHA YA UTAKATIFU NA UTAUWA
Hili ni eneo la pili la muhimu ambalo mwamini inampasa kuishi katika namna ya kujikana kama kukubali ule wito aliotupa yesu katika "Luka9:23-24"

Neno "utakatifu" na neno "utauwa" ni maneno ambayo yamekuwa yakitumika kama neno lenye maana moja lakini yana utofauti kidogo ila yanafika kuwa na shabaha moja.

Maana ya utawa
Utauwa ni hali ya kujitoa ki-Mungu ambayo huambatana na kuongezeka kwa uchaji mbele za Mungu.

Matendo ya Mitume 10:1-2 "Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima."

Ukisoma sura ya 10 yote ya Matendo utagundua Kornelio alikuwa ni mtu ambaye ana mtolea Mungu Ibada, akiwa amejaa uchaji lakini hakuwa mtakatifu yani alikuwa Muungwana na ndio maana huyu mtu ilipaswa aletewe Petro ili amsaidie afikie katika utakatifu kabisa. Kwahiyo mtu anaweza kuwa mtauwa lakini asiwe mtakatifu. Kwahiyo kuwa mtauwa huwa kunaleta kibali na kukubaliwa na Mungu πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Matendo ya Mitume 10:34-35
"Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye."

Sasa Embu tuangalie zaidi kwenye eneo hili zaidi kidogoπŸ‘‡πŸ‘‡
1 Timotheo 3:16 "Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu."

Ukisoma maandiko hapo juu unaona namna Paulo anavyomwaambia Timotheo kwamba utauwa una siri kubwa halafu anaanza kueleza namna ambavyo Yesu alijitoa na kufanya kazi ambapo inatujengea msingi mkuu katika kuelewa kwamba Utauwa unaambatana na kujitoa katika kristo Yesu.

1 Timotheo 6:5
"na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida."

Watu huwa wanamcha Mungu ili kupata faida zao binafsi lakini wangejijenga kujitoa ili waupate utakatifu ingekuwa na maana sana na ndio maana paulo alikuwa anatamani sana Timotheo ajiepushe na hao watu wa namna hiyo maana hawafiki kwenye kina cha moyo wa Mungu cha utakatifu.

Katika hayo yote Yesu pia alitamani tuweze tuongezeke katika kumcha Mungu kwa kujitoa kwetu siku zote za Maisha yetu tunapokuwa chini ya Jua hapa. Kaa chini angalia ni kwa namna gani ambavyo umejikana kwa ajili ya kristo na uishi kwa namna gani ili uwe sahihi mbele za Mungu.

Maana ya "Utakatifu"
Utakatifu ni "hali ya usafi wa kiroho, nafsi na kimwili".

Asili ya neno "utakatifu"
Neno "utakatifu" linaweza kuelezewa kutoka kwa maneno mawili, neno la kiebrania na neno la kigiriki
✍️Neno "utakatifu" limetokana na neno la kiebrania "Qadash" likiwa na maana "kujitenga au kutengwa kwa usafi"
q
✍️Neno "utakatifu" linaweza elezewa na neno la kigiriki "Hagios" likimaanisha "kutokuwa na makosa au udhaifu au uchafu"

Mungu anatamani watu wote waliokubali kumuishia waishi maisha ya utakatifu haijarishi mazingira yake yako magumu vipi hata kama pia yanamshawishi yeye kuingia katika dhambi ila kwa ajili ya Mungu anatutaka kuwa na maisha ya utakatifu na sio kitu kingine chochote.

Mambo ya Walawi 19:2
"Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu."

1 Petro 1:15-16,22 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu."


Mungu alimwambia Musa awakumbushe wana wa Israel kwamba inatakiwa waishi maisha ya utakatifu maana yeye ni mtakatifu ndio vivyo hivyo hata kwetu kwamba tukijikana kwa ajili ya kristo Yesu basi tutakuwa tayari kuyaishi maisha ya utakatifu siku zote maana Yesu mwenyewe ni mtakatifu na sisi inatakiwa tuwe hivyo maana Yeye katika kuishi kwake hakufanya dhambi. Ona hapo chiniπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

1 Petro 2:22
"Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake."

Kama yeye hakufanya dhambi basi nasi lazima tuufuate mfano wake ili tuwe tumejikana kikamilifu na kumfuata namna ambavyo alikuwa amesema tumuishie.

N.B: Huwezi kuutenganisha Utakatifu na Utauwa hata siku moja kama kweli wewe umemaanisha kujikana kwa ajili ya Yesu kristo Yesu. Utakatifu ni hatua ya juu inayofuata baada ya mtu kuwa amekuwa mchaji mzuri aliyejitoa kikamilifu mbele zake.

Mambo muhimu juu ya Utakatifu na utauwa ya kuyabeba kama MwaminiπŸ‘‡πŸ‘‡
✍️✍️✍️Usije ukajiachia hata siku moja maana utakatifu huwa unatafutwa na sio suala la dakika moja bali linaitaji kujengwa kuanzia msingi wa wewe kumjua na kumuelewa Mungu.πŸ‘‡πŸ‘‡

Waebrania 12:14 "Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;"

✍️✍️✍️ Lazima ujizoeze kuuishi utakatifu na Utauwa siku zote hata kama unaona mazingira yanakuwa magumu kwako huko ndiko kutakufanya kujikana kikamilifu wakati wote.

1 Timotheo 4:7-8 "Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye."

✍️✍️✍️Pia lazima ufike hatua ujue ya kwamba utakatifu unahusisha mwili, nafsi pamoja na Roho. Sasa kama wewe uko tayari kwenda na Mungu lazima ujue kuishi utakatifu katika maeneo yote hayo matatu.

1 Wathesalonike 5:23
"Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo."

✍️✍️✍️ Jifunze kuwa mtu wa kusoma neno na kulitafakari neno la Mungu, kuwa mtu wa maombi n.k ndipo utaweza kuyaishi maisha ya utakatifu. Unaweza soma vifungu hivi (Yoshua1:9, Mithali 4:20)

Mungu akubariki kwa kuambatana nami katika sehemu hii ya kwanza. Natumaini ya kwamba Utaenda pamoja nami sehemu ya pili ambayo pia itakuwa hapa karibuni kupitia Mitandao yangu ya kijamii. 
Mungu akubariki sana
Ulikuwa nami mpendwa wako katika kristo
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com