Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema 1KORINTHO 15:33

KUJIKANA NDANI YA KRISTO YESU (Sehemu ya kwanza)


Bro Jackobo


Utakuwa nami mpendwa katika kristo yesu
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com

UTANGULIZI
Katika kizazi hiki cha Utandawazi (Sayansi na teknolojia) Tumekuwa na kanisa ambalo limekuwa likienda pasina utaratibu huku likijiona kukamilika sana kuliko hata Yesu kristo mwenyewe. Watu wamekuwepo nyumbani mwa Mungu lakini Dhambi kwao ni kitu cha kawaida wala hawana hata Hofu kidogo na wanajiona ya kuwa wako katika msitari wa Mungu huku wakipuuza maagizo yake. Mungu anatafuta moyo wa mtu ambaye amekubali kuacha mambo yote kwaajili yake na ndio maana Mungu kanipa kuleta hili Somo "Kujikana Ndani ya kristo Yesu" liweze kutusaidia ili tubaki katika msingi wa Ki Mungu ambao yeye ameukusudia tuweze kuishi katika huo.

Somo letu limegawanyika katika maeneo makuu sita yanayomfanya huyu mtu aweze kujikana kikamilifu ndani ya kristo Yesu. Karibu tuambatane kwa pamoja ili tuweze kuelewa kiundani zaidi.

Maeneo Muhimu ya somo Letu.
1. Maana ya Kujikana Ndani ya Yesu kristo
2. Mwanzilishi /Mwasisi wa Kujikana
3. Maeneo Muhimu mwamini anapaswa kujikana
4. Vipingamizi kwa kanisa katika kujikana kwa Kristo Yesu
5. Madhara yanayoweza kutokea kwa kanisa kushindwa kujikana Mbele za Yesu Kristo
6. Mambo ya kumsaidia Mwamini kumaanisha kujikana kwake.




1. MAANA YA KUJIKANA NDANI YA YESU KRISTO
Neema ya Mungu imefunuliwa kwetu kiasi kwamba inatuelekeza Yenyewe namna ya kupata maarifa sahihi katika neno lake na ndio maana anasema Yeye ni Mungu ambaye huwa anatufundisha tuweze kupata faida πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Isaya 48:17 "BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata."

Sasa ni nini maana ya kujikana ndani ya Yesu kristo? Tunamaanisha nini tunaposema huyu mtu amejikana kwaajili ya Yesu kristo? Je kila ambaye ameokoka amekwisha kujikana ndani ya kristo Yesu? Je ipo siri gani tunayotakiwa kuishika au kuiishi ili tuwe tumejikana ndani ya Yesu kristo?

Kujikana ndani ya Yesu kristo ni hali ya kuacha mambo yako yaliyokuwa na heshima, ufahari na kukupatia faida kwa ajili ya kufanya mapenzi na makusudi ya Mungu kupitia kristo Yesu.

Kwa mwamini Yeyote yule ni lazima mambo yote anayoyafanya yapitie kwa kristo Yesu ili aweze kupata uhalali na haki yaani kifupi haki ya mwamini yeyote mbele za Mungu ipo ni kwasababu Yesu kristo amesimama na ndio maana kuyafanya mapenzi ya Mungu ni lazima tupitie kwa Yesu kristo kwakuwa Yeye ndiye njia ya kweli na uzima na hakuna anayeweza kumwona Mungu bila yeyeπŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 14:6 ,"Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi."

Sasa kuna andiko la msingi hapa linalobeba Somo letu la siku ya Leo ambalo ndio funguo la yote tutakayojifunza kwenye huu Mfululizo wa somo hiliπŸ‘‡πŸ‘‡

Luka 9:23-24 "Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha."

Ukiangalia hapo Yesu alipokuwa akisema na wanafunzi wake alikuwa anawaandaa katika hali ya kumuishia Mungu katika mantiki ya kwamba wayahesabu mambo yao sio ya maana bali waone kwamba mambo ya Kristo Yesu ndio ya maana zaidi. Hii ilimfanya ifike wakati sasa awaambie wajikatae/kujikana ili kwamba wamfuate Yesu na huku wamebeba mizigo/msalaba/mateso yao. Mungu alikuwa anawafundisha namna ya kutoa kipaumbele mambo yote yanayomhusu Mungu na sio yazifurahishazo nafsi zao hata kidogo. Hapa pia alikuwa akiwaonyesha kwamba katika kristo sio kwamba watapata kufurahi tu bali hata mateso yangewakuta kwaajili yake.

Mtu anapoamua kujikana kwa ajili ya Yesu kuna kuwa na tabia au mwenendo ambao anapaswa kuuacha na kuambatana na mwenendo au tabia atakayoambiwa baada ya kukubali wito wake. Kuacha tabia zako ulizokuwa nazo sio kitu rahisi hata kidogo kwasababu ya uraibu unaokuwa umejijenga kwa hizo tabia. Mfano kwa vijana ambao huwa wanajichua au wanafanya Punyeto (masterbation) huwa sio rahisi sana kuacha kwasababu kuna kumbukumbu linalo waendesha ndani yao litokanalo na kemikali ndani ya mwili iitwayo Dopamine inayomsukuma kurudia ili aweze kupata ile furaha (pleasure) aliyowahi kuipata. Kwahiyo ili aweze kuacha lazima kuwe na nguvu ya kumsaidia huyu mtu ambayo imefungwa ndani ya kristo ambapo anataka sasa tuende na mizigo (tabia) Yetu ili aweze kutupumnzisha (kutuondolea).πŸ‘‡πŸ‘‡

Mathayo 11:28-30 "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi."



2. MWANZILISHI/MWASISI WA KUJIKANA.
Nani alikuwa mwanzilishi wa kujikana??
Note: Mwanzilishi mkuuu wa kujikana alikuwa ni Yesu mwenyewe kwa namna ambavyo aliacha Enzi na utukufu wake akaja kutuokoa sisi. Na aliona kwamba ile heshima na utukufu wa ki-Mungu sio kitu cha maana ila kukamilisha ule wito au kule kukubali kwake kujitoa kwa ajili ya maisha yetu hata ukafika hatua akawa yuko tayari kunyenyekea hata mauti ili aweze kutupata sisi ambao tulikuwa tumepotea.

Wafilipi 2:5-7
"Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;"


Pia Yesu aliweza kutuchagua sisi licha ya kwamba tulikuwa na dhambi ili kwamba atufanye sisi tuwe wana wa Pendo lake na sio sisi tuliomchagua yeye. Sasa huku kwa yeye kutuchagua kunaonyesha kujikana kwake mbele ya Mungu baba ambako pia ndio mfano tunatakiwa kuufuata.

Yohana 15:16
"Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni."

Katika kujitoa/kujikana kwa Yesu kristo ndiko ambako mwamini inatakiwa afuate mfano wake na sio mfano wa mwanadamu awaye yeyote. Hii ilimfanya mpaka atupe uhakika wa kuweza kufanya mambo ambayo ameyafanya na zaidi ya yale aliyokuwa ameyafanya. Ona hapa ambapo alituthibitishia ili kwamba tukiwa na hekima na maarifa ya Ki-Mungu tuweze kufuata njia yakeπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 14:12
"Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba."

3. MAENEO MUHIMU AMBAYO MWAMINI ANATAKIWA KUJIKANA NDANI YA KRISTO
A. Utumishi
B. Maisha ya utakatifu na utauwa.

A. UTUMISHI
hii ni hali ya kuwa na utayari wa ndani wa kutekeleza majukumu/maagizo ambayo Bwana wako amekupa ili uweze kuyatekeleza.
Utumishi ambao Yesu ameuweka kwa mwamini ambaye amechagua kuwa na Yeye huwa umejikita sana katika maeneo haya
A. Kuitwa
B. Kutumwa
C. Utekelezaji

A). KUITWA: ili kuenda kutekeleza majukumu ya Mungu lazima akuite kutoka katika majukumu uliyo nayo na kuyaacha ili uyafanye mapenzi ya Mungu aliyekuita. Ukiwa kama mtu unayetaka kujikana kwa ajili ya Kristo Yesu usije ukaingia kwenye utumishi kisa umekosa kazi ya kufanya bali acha kazi yako ili uweze kumtumikia Mungu na ndio maana yeye alio waita waliacha walivyo navyo ili wamaanishe kule kuacha kwao πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mathayo 4:18-22 "Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata."

B. KUTUMWA: Watu wengi huwa wanasikia sauti ya Mungu ikiwaita kwenye utumishi lakini huwa wanakurupuka kwenda kutumika pasina kupokea maelekezo Mungu anayotaka wewe uyaishi katika eneo lako. Kwahiyo lazima ujifunze kuelewa sauti ya Mungu katika utumishi wako ili kujitoa kwako kwake kuwe na maana. Muone mtumishi wa Mussa alichokifanyaπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Kutoka 3:10-12
"Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu."

Ilikuwa inatosha tu kwa Musa kuondoka kwenda kuwatoa wana wa Israel lakini alitaka kupata taarifa kiundani zaidi ili hata kama akiulizwa kitu awe na majibu ya kuwapa. Usiende kufanya kazi ya Mungu pasina kuwa na maelekezo kamili ya Mungu aliye kuita maana ile kazi utaifanya sio kazi yako wewe bali ni ya yeye aliyekutuma kwenda kuifanya hiyo kazi ya Mungu.

C. UTEKELEZAJI: sasa hapa ndipo ambapo huyu mwamini anakamilisha kile kitu ambacho Mungu anataka akifanye. Lazima huyu mwamini akubali kufanya kazi ya Mungu haijalishi hali yake itakuwa inamuambia nini, hata kama unajiona huwezi lakini hapa lazima uyatekeleze yale ambayo Mungu amekupa kuyafanya na uyaache yale kwako unaona yana umuhimu ili jina la Bwana litukuzwe kupitia utumishi wako wa kila siku.

Wafilipi 3:7-8
"Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;"

Paulo kwa ajili ya kristo aliamua kupata hasara ili aweze kumpendeza kristo ambaye alimuita ili aweze kumtumikia yeye na huku ndiko kujikana ambapo Kristo alitamani wanafunzi wake wawe kama namna ambavyo paulo alikuwa tayari kuingia gharama/Hasara (Kuna gharama katika kumtumikia Mungu ambayo mwamini lazima akubali kuibeba). Paulo aliacha mshahara na marupurupu mbalimbali kutoka kwenye dini ya kiyahudi ili aweze kumpendeza Mungu.

Siku zote kama mwamini lazima ufike hatua na kuwa na utayari wa kuacha yote ili uweze kuitimiza ile kazi ambayo Mungu amekupa wewe kuifanya kama vile ambavyo paulo alifanya. Pia ukitaka kuelewa hata Petro ilibidi amuulize Yesu kwamba itakuwaje maana tumeacha yote nini kwako tutapata.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mathayo 19:27-29 "Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele."

Unapokubali sasa kujikana kwaajili ya ktisto ni lazima sasa ukubali kutii yale ambayo Yesu aliyasema. Ndio maana Yesu alipokuwa anaondoka aliwaambia wanafunzi juu ya utumishi katika kuieneza injili yake na sio vinginevyo. Na alitamani wanafunzi wake wawe hivyo onaπŸ‘‡πŸ‘‡

Marko 16:15
"Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe."

Sasa wewe uliye tayari kuwa na Mungu lazima ukubari kuihubiri injili kwa mazingira yawayo yoyote ili kuonyesha utayari wako kumtumikia Mungu katika eneo ambalo amekupa uweze kutumika.

Usikubali kukaa tu ndani ya nyumba ya Mungu pasina kuwa na kazi yeyote lazima uwe tayari kuifanya ile huduma ambayo Mungu amekupa wewe.


B. MAISHA YA UTAKATIFU NA UTAUWA
Hili ni eneo la pili la muhimu ambalo mwamini inampasa kuishi katika namna ya kujikana kama kukubali ule wito aliotupa yesu katika "Luka9:23-24"

Neno "utakatifu" na neno "utauwa" ni maneno ambayo yamekuwa yakitumika kama neno lenye maana moja lakini yana utofauti kidogo ila yanafika kuwa na shabaha moja.

Maana ya utawa
Utauwa ni hali ya kujitoa ki-Mungu ambayo huambatana na kuongezeka kwa uchaji mbele za Mungu.

Matendo ya Mitume 10:1-2 "Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima."

Ukisoma sura ya 10 yote ya Matendo utagundua Kornelio alikuwa ni mtu ambaye ana mtolea Mungu Ibada, akiwa amejaa uchaji lakini hakuwa mtakatifu yani alikuwa Muungwana na ndio maana huyu mtu ilipaswa aletewe Petro ili amsaidie afikie katika utakatifu kabisa. Kwahiyo mtu anaweza kuwa mtauwa lakini asiwe mtakatifu. Kwahiyo kuwa mtauwa huwa kunaleta kibali na kukubaliwa na Mungu πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Matendo ya Mitume 10:34-35
"Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye."

Sasa Embu tuangalie zaidi kwenye eneo hili zaidi kidogoπŸ‘‡πŸ‘‡
1 Timotheo 3:16 "Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu."

Ukisoma maandiko hapo juu unaona namna Paulo anavyomwaambia Timotheo kwamba utauwa una siri kubwa halafu anaanza kueleza namna ambavyo Yesu alijitoa na kufanya kazi ambapo inatujengea msingi mkuu katika kuelewa kwamba Utauwa unaambatana na kujitoa katika kristo Yesu.

1 Timotheo 6:5
"na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida."

Watu huwa wanamcha Mungu ili kupata faida zao binafsi lakini wangejijenga kujitoa ili waupate utakatifu ingekuwa na maana sana na ndio maana paulo alikuwa anatamani sana Timotheo ajiepushe na hao watu wa namna hiyo maana hawafiki kwenye kina cha moyo wa Mungu cha utakatifu.

Katika hayo yote Yesu pia alitamani tuweze tuongezeke katika kumcha Mungu kwa kujitoa kwetu siku zote za Maisha yetu tunapokuwa chini ya Jua hapa. Kaa chini angalia ni kwa namna gani ambavyo umejikana kwa ajili ya kristo na uishi kwa namna gani ili uwe sahihi mbele za Mungu.

Maana ya "Utakatifu"
Utakatifu ni "hali ya usafi wa kiroho, nafsi na kimwili".

Asili ya neno "utakatifu"
Neno "utakatifu" linaweza kuelezewa kutoka kwa maneno mawili, neno la kiebrania na neno la kigiriki
✍️Neno "utakatifu" limetokana na neno la kiebrania "Qadash" likiwa na maana "kujitenga au kutengwa kwa usafi"
q
✍️Neno "utakatifu" linaweza elezewa na neno la kigiriki "Hagios" likimaanisha "kutokuwa na makosa au udhaifu au uchafu"

Mungu anatamani watu wote waliokubali kumuishia waishi maisha ya utakatifu haijarishi mazingira yake yako magumu vipi hata kama pia yanamshawishi yeye kuingia katika dhambi ila kwa ajili ya Mungu anatutaka kuwa na maisha ya utakatifu na sio kitu kingine chochote.

Mambo ya Walawi 19:2
"Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu."

1 Petro 1:15-16,22 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu."


Mungu alimwambia Musa awakumbushe wana wa Israel kwamba inatakiwa waishi maisha ya utakatifu maana yeye ni mtakatifu ndio vivyo hivyo hata kwetu kwamba tukijikana kwa ajili ya kristo Yesu basi tutakuwa tayari kuyaishi maisha ya utakatifu siku zote maana Yesu mwenyewe ni mtakatifu na sisi inatakiwa tuwe hivyo maana Yeye katika kuishi kwake hakufanya dhambi. Ona hapo chiniπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

1 Petro 2:22
"Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake."

Kama yeye hakufanya dhambi basi nasi lazima tuufuate mfano wake ili tuwe tumejikana kikamilifu na kumfuata namna ambavyo alikuwa amesema tumuishie.

N.B: Huwezi kuutenganisha Utakatifu na Utauwa hata siku moja kama kweli wewe umemaanisha kujikana kwa ajili ya Yesu kristo Yesu. Utakatifu ni hatua ya juu inayofuata baada ya mtu kuwa amekuwa mchaji mzuri aliyejitoa kikamilifu mbele zake.

Mambo muhimu juu ya Utakatifu na utauwa ya kuyabeba kama MwaminiπŸ‘‡πŸ‘‡
✍️✍️✍️Usije ukajiachia hata siku moja maana utakatifu huwa unatafutwa na sio suala la dakika moja bali linaitaji kujengwa kuanzia msingi wa wewe kumjua na kumuelewa Mungu.πŸ‘‡πŸ‘‡

Waebrania 12:14 "Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;"

✍️✍️✍️ Lazima ujizoeze kuuishi utakatifu na Utauwa siku zote hata kama unaona mazingira yanakuwa magumu kwako huko ndiko kutakufanya kujikana kikamilifu wakati wote.

1 Timotheo 4:7-8 "Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye."

✍️✍️✍️Pia lazima ufike hatua ujue ya kwamba utakatifu unahusisha mwili, nafsi pamoja na Roho. Sasa kama wewe uko tayari kwenda na Mungu lazima ujue kuishi utakatifu katika maeneo yote hayo matatu.

1 Wathesalonike 5:23
"Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo."

✍️✍️✍️ Jifunze kuwa mtu wa kusoma neno na kulitafakari neno la Mungu, kuwa mtu wa maombi n.k ndipo utaweza kuyaishi maisha ya utakatifu. Unaweza soma vifungu hivi (Yoshua1:9, Mithali 4:20)

Mungu akubariki kwa kuambatana nami katika sehemu hii ya kwanza. Natumaini ya kwamba Utaenda pamoja nami sehemu ya pili ambayo pia itakuwa hapa karibuni kupitia Mitandao yangu ya kijamii. 
Mungu akubariki sana
Ulikuwa nami mpendwa wako katika kristo
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com


14 comments:

  1. Barikiwa sana mtumishi

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ubarikiwe sana mtumishi hakika somo nimelielewa

      Delete
  2. Mungu akubariki Sana kwa ujumbe huu mzuri

    ReplyDelete
  3. Ubarikiwe sana mtumishi

    ReplyDelete
  4. Amen minister πŸ™

    ReplyDelete
  5. Ubarikiwe sana mtumishi WA Mungu

    ReplyDelete
  6. Asantee, Ubarikiwe sana mtumishi wa Mungu

    ReplyDelete
  7. Ubalikiwe mtumishi wa mungu

    ReplyDelete
  8. Be blessed servant of God. I have learnt something new from this good lesson. Keep it up

    ReplyDelete
  9. Amina. Mungu akubariki sana sana

    ReplyDelete
  10. Vizuri sana mtumishi elimu nzuri.
    Lakini n vigumu katika Karne kupata mtu wa kusoma hizo paragraph zote isipokuwa awe n mtu wa kusoma n.k nakushauri hizi contents zakouwe unazitenhenezsa video pia

    ReplyDelete
  11. "Watu wengi huwa wanasikia sauti ya Mungu ikiwaita kwenye utumishi lakini huwa wanakurupuka kwenda kutumika pasina kupokea maelekezo Mungu anayotaka wewe uyaishi katika eneo lako"

    Mungu ni mwema sana, Asante kwa neno hili la Mungu kwangu ambalo Roho Amelia hiari kwangu, ni dhahiri halijaja bure kwangu, na heri nijichunguze zaidi kuna mahali tu speed ya kujitoa kwangu itakua imepungua au haipo kabisa,

    Mungu anirehemu na kutusaidia,
    Kristo Yesu akubariki sana Ndugu

    ReplyDelete