USIKATE TAMAA WALA KUVUNJIKA MOYO WAKATI WA MUNGU HAUWEZI KUTABILIWA KWA AKILI ZA KIBINADAMU


Bro Jackobo

Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email: jackobombwaga@gmail.com


Bwana YESU asifiwe mwana wa MUNGU karibu tujifunze neno la MUNGU juu ya hili somo ili kwamba tuweze kuelewa utendaji wa MUNGU kwenye maisha ya mwanadamu ili kuweze kuwa na Tumaini kubwa na yeye hata kama mambo magumu yametusonga sana na hatuoni kuendelea lakini kupitia somo hili nakuambia BADO LIPO TUMAINI LAKUSHINDA NA KUTOKA KWENYE HAYO MATESO YAKO

UTANGULIZI
Watu wengi sana wamefika wakati wanatamani sana kutumia akili zao katika kujua hatima za siku za maisha yao ya kiuchumi, kijamii, kisiasa Kifamilia (ndoa) na hata kiroho pia kiasi kwamba imefika hatua wamemuweka Mungu pembeni wanajiongoza wenyewe kwa akili zao.
Lakini leo napenda nikukaribishe tujifunze kwa pamoja juu ya somo hili ambalo kichwa chake kinajitosheleza kabisa kwamba “USIKATE TAMAA WALA KUVUNJIKA MOYO WAKATI WA MUNGU HAUWEZI KUTABILIWA KWA AKILI ZA KIBINADAMU”
Kabla hatujaendelea ningependa niweke msingi kidogo juu ya somo katika maandiko haya

ISAYA 40;28 
Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki”.

Kama Mungu atakupa neema ya kuelewa jambo kwenye maisha yako inakupasa umtukuze na kumuinua maana kama hataruhusu uweze kuelewa jambo hilo hautaliweza kulielewa ndio maana huwezi kuzichunguza akili zake hata siku moja yeye yuko juu sana zaidi ya tunavyoweza kuwa tunafikiri.

Pia lazima utambue ya kwamba endapo Mungu atakusudia kufanya jambo kwa mtu lazima kuna kusudi nyuma yake ambalo Mungu huwa anampa huyo mtu kwamba alifanye au atengeneze

YOHANA 9;1-3
“ Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, Ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake” 

Wanafunzi wa Yesu walifikiri kwa akili zao wenyewe wakajiona ya kwamba wao kwa sababu hawakuwa vipofu basi walikuwa katika haki mpaka wakamuuliza kwamba nani alifanya dhambi mpaka huyu akawa kipofu kumbe Yule kipofu kuma jambo Mungu aliweka nyuma ya pazia ambalo ilikuwa ngumu kwa mtu kutambua.

Japo wanafunzi wa Yesu hawakukosea sana kulinganisha na namna ya kufikiri kwao kwasababu wakati mtu akimuacha Mungu basi yeye Mungu huruhusu magumu yampate Yule aliye simama vizuri akaanguka. Kumbuka pia hata shetani huwa hawezi kumuacha mtu aliye mtesa mwanzo hivihivi pasipo kumtesa endapo ataanguka baada ya kuuacha wokovu. Kwahiyo usiruhusu nafasi ya kuanguka alafu ukategemea Mungu yuko na wewe katika hayo magumu unayoyapitia. TUNZA UTAKATIFU KWANZA.

Unaweza ukawa unajiuliza kwanini napitia magumu au kwanini kila wakati naona kutokuendelea mbele katika maisha yangu? Usiogope endapo ukigundua umekaa vizuri na Mungu jua ya kwamba kuna kitu nyuma ya pazia ambacho inakupasa ukifanye au Mungu anataka kujitukuza kupitia wewe. Japo ni ngumu sana kumuelewa Mungu ikiwa amekuruhusu upite kwenye mateso ndio maana nakwambia “hauwezi kuzichunguza akili za Mungu kwa akili za kibinadamu” unamuhitaji Mungu akufundishe na akufunulie uweze kuelewa


KIINI KATIKA SOMO
2 PETRO 3:8-9 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”

Maandiko hayo hapo juu yanatupa mwongozo wa namna ya utendaji wa Mungu katika maisha ya mwaminini kwamba Mungu huwa anafanya pale ambapo anaona yeye mwenyewe kwamba panafaa kufanyika jambo.
Unaweza ukawa unapitia mazingira magumu sana kwenye maisha yako kiasi kwamba ukashindwa kuelewa Mungu anakuwazia nini na anampango gani na wewe lakini nikutie moyo kwamba Mungu yeye katika yote huwa anafanya kwa wakati na magumu yako bado anayajua na kuyaona huna haja ya kuvunjika moyo wala kukata tama bado tumaini lipo katika kristo Yesu
Mbona unajaribu kukata tamaa ya kumtafuta Mungu usivunjike moyo Mungu atafanya kwa wakati wake hauhitajiki kutumia akili zako wewe mruhusu Roho Mtakatifu achukue nafasi moyoni mwako ataweza kukuelekeza nyakati sahihi za Mungu kwenye maisha yako. 

Suleimani anatuonya kupitia 👇👇👇
 Mithali 24:10 
"Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.” 

Sasa mwana wa Mungu inakuwaje unakata tama ya kuendelea na wokovu wakati unapita kwenye magumu? Inakuwaje unaacha kumtumainia Mungu wakati unapita kwenye magumu? Tambua kwamba pale unapopitia magumu ndipo unakuwa na nguvu kidogo za kuweza kushinda ndio maana una mhitaji Mungu zaidi
Kumbuka Yesu wakati wa kukinywea kikombe cha mateso alifanyaje, Yesu licha ya kwamba alikuwa Mungu bado aliingia kumtafuta MUNGU (nafsi ya Baba) ili kwamba aweze kumsaidia aweze kumshindia kuyavumilia mateso yale na ikiwezekana kile kikombe cha mateso kimuepuke ndio maana malaika alikuja kumtia Nguvu👇👇

Luka22;43 
"Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu"

 sasa wewe kwanini ukate tama kwenye tatizo lako na ni kwanini utamani kuenda kwa waganga wa kienyeji wakati Mungu yupo? Lipo tumaini huwezi kumuelewa Mungu hata siku moja ikiwa unataka kuchunguza sana kwa kutumia akili zako kujua wakati wa kujiliwa kwako.

2PETRO2:9-10 basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka.”

Biblia inajieleza wazi kwamba yeye ndiye ambaye anawaokoa watu wake na majaribu, ndugu yangu magumu pamoja na changamoto zako Mungu anaweza akakutoa katika hizo na akakuokoa akakuweka huru shida ni wewe kutokutaka kumsikiliza Mungu. Kuna mwimbaji (Ambwene Mwasongwe) ameimba wimbo huu kwamba tatizo haliko kwa Mungu bali tatizo liko kwetu wanadamu na ndio maana nakutia moyo inuka tena Mungu anaweza kukutoa hapo ulipo akakupa kuketi sehemu ya starehe wewe subiri tu wakati wa Mungu usione kama Mungu kachelewa kutimiza ahadi yake ya kuponya na kukutoa hapo ulipo.

Lakini nikukumbushe  pia biblia imesema kwamba huwaweka wasio haki katika hali ya adhabu sasa usimfanye Mungu akupe adhanu kwa moyo wako wa kutokumuamini juu ya utendaji wake tena adhabu yako inaweza ikakufanya ukafirisika kiroho na kimwili.  Usikubali kuufuata mwili namna unavyokushurutisha bali liishi neon la Mungu utakuwa na usalama kwenye maisha yako lasivyo utakuwa unajidanganya hauwezi kumuona Mungu hata siku moja ndugu yangu.

Kumbuka Mungu hapendi mtu awaye yeyote apotee ndugu yangu na ndio maana nakuambia unapopita kwenye magumu usiwe mwepesi wa kuona kama Mungu amekuacha bado yeye yuko pamoja na wewe na atakuokoa siku ya mateso yako kwasababu yeye ndiye anajua namna ya kukutoa katika mateso ambayo umayapitia, sijui unapita kwenye mateso gani wala unapita kwenye shida ipi lakini moja nilijualo ya kwamba Mungu ni Mungu wa yasiyowezekana kwa akili zetu za kibinadamu.

MAOMBOLEZO 3:25-27, 31 
“Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo. Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake. Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.”

Ukimngoja Bwana yani ukawa na subira juu ya Bwana lazima Bwana ataonyesha wema wake kwako hatokuacha hivyohivyo ulivyo mpendwa lazima atakutokea katika hali yako uliyo nayo tena atakupa hatua moja nyingine zaidi ya kumtafuta na ukawa huru katika teso la Moyo wako.

Lazima ufungiwe nira na kristo. Nira huwa ni kipande cha mti ambacho Ngombe au farasi hufungwa wakati akiwa analima.

 Kwahiyo unapozungumzia Nira unamaanisha USHIRIKA AU MAHUSIANO kwahiyo lazima uwe na wakati mzuri wa kutengeneza mahusiano yako na Mungu ili aweze kuendelea kuonyesha wema wake katika maisha yako. Na  kwa upande wa vijana biblia inatusisitiza kujenga mahusiano yetu mazuri na Mungu maana ukiwa na wakati mwema wa ujana una nafasi kubwa ya kumshinda adui maana utakuwa nazo nguvu kama vile maandiko yasemavyo kwamba vijana tunazo nguvu. Lakini usitegemee kama Mungu atahusika na ,maisha yako endapo utakuwa na mahusiano mabovu na Mungu wa mbinguni aliye hai.

Bado naendelea kukusisitiza kwamba haya mambo yanahitaji akili njema ya kiroho iliyopevuka kuweza kuyaelewa. Mungu siyo wa mchezo yeye ni mtakatifu kwa hiyo ni vizuri kama utajenga sana vema mahusiano yako na Mungu ndipo utaona siku zako zina heri na tena hautakata tamaaa kwenye maisha yako.

Note:Kuwa mtumishi isikupe kiburi ya kwamba basi nimeshashinda tayari na kwamba siwezi nikakata tamaa, 

Ngoja nikukumbushe Eliya alikuwa nabii wa Mungu mkubwa sana lakini alitishwa na maneno madogo tu ya kwamba atauawa akasahau ya kwamba Mungu ndiye alimshindia katika Mengine yote.
Utumishi wako kanisani uwe ni chachu ya kukuwezesha kumtafuta Mungu na nguvu zake zijazo pia kuwa mtumishi sio tiketi ya kwamba wewe ushakuwa mtakatifu na unauwezo wa kustahimili ila ukijazwa na Roho Mtakatifu ndiye atakusaidia mpendwa. Hauna haja ya kukata tamaa maana Mungu yuko kwa ajili yako.

Roho mara nyingi huwa iko tayari kuvumilia yote lakini mwili huwa hauko tayari kuvumilia sasa ngoja nikuambie kitu kwamba kama utakuwa na nguvu sana za kiroho basi utaweza kuisikiliza Roho lakini kama utakuwa na Nguvu nyingi za mwilini kuliko za Rohoni tambua ya kwamba wewe basi utaufuata mwili.
Ushauri yatafute sana Mambo ya rohoni huo ndio msingi mkubwa wa mafanikio ya maisha ya kiroho na ustahimilivu katika magumu

YOSHUA 1:6-8 
Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana

Hakuna mtu awaye yeyote atakaye sitawi pasipo kukaa kwenye torati za Mungu tena hakuna atakaye weza kuvumilia magumu na changamoto asipokuwa na torati ndani yake pamoja na ujasiri. Kwahiyo ili uweze kushinda lazima uwe na ujasiri wa kushinda vita yeyote, huwa ushindi unaanza katika mawazo na ndio maana hata wanajeshi wakiwa katika vita huwa wanakaa kwanza chini na kupanga mikakati ni namna gani wanaweza kushindi ndipo waingie kwenye utendaji wa vitendo.

Mtazamo wako unaweza ukakukwamisha kukutana na na Mungu kwa namna moja ama nyingine endapo tu utataka uzichunguze njia za Mungu kwa kutumia akili zako katika utendaji wake kwenye magumu au changamoto wewe  kazi yako ni kumuomba Roho mtakatifu akusaidie uweze kushinda kwenye maisha yako pamoja na changamoto mbalimbali zinazokukabili kwenye maisha yako.


MAMBO AMBAYO HUWAFANYA WATU WAKATE TAMAA KWENYE MAISHA YAO JUU YA MAGUMU WANAYOYAPITIA MPAKA WASIELEWE WAKATI WA MUNGU

1. KUKOSA KUMJUA MUNGU VIZURI KATIKA MAISHA YAO

Kuingia kanisani hakumpi mtu tiketi ya kumjua Mungu na sio kila unaye muona yuko kanisani kwamba atakuwa anamjua Mungu wengine wapo kanisani kwa mda mrefu lakini bado hawajafika viwango vya kumjua na kumuelewa Mungu na ndio maana ni rahisi sana wakakata tamaa maana hayupo wa kuwaelekeza vitu vya msingi kwenye maisha yao

WAEBRANIA 11;6 
“Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”

YAKOBO 2:14-17 
“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi Na kupungukiwa Na riziki, Na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu Kwa amani, mkaote moto Na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake”

Ili ifike mtu tuseme anamjua Mungu lazima maisha yake yafike yawe na uhalisia katika matendo hakuna mtu anaweza kusema mimi niko na wewe wakati wote na wewe ukaamini wakati unaona yuko mbali na wewe kwahiyo katika kumjua Mungu lazma uhakikishe umefika kwenye viwango vya kuwa na Tunda la ROHO (UPENDO) pamoja na madhihirisho yake kama utu wema, uvumilivu, upole, kiasi n.k (WAGALATIA 5;22)

AYUBU 22:21 
“Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.”

Ili uweze kuvumilia na kumsubiri Mungu lazima uwe umefika viwango vya kumjua na kumuelewa Mungu vizuri kwenye maisha yako lasivyo utakuwa unajidanganya. Pasipo kuwepo na amani huwezi kuvumilia magumu hata siku moja kwa hiyo lazma utafute amani na ni Yesu pekee anaye weza kukupa amani kwenye maisha yako ya kila siku.

Kumbuka ukiwa unapita kwenye magumu na mambo ya kuumiza huwa mara nyingi amani inatoweka lakini ukimtazamia Mungu atakupa amani moyoni mwako itakayo kuwa chachu ya wewe kuweza kuvumilia magumu yote. Ayubu asingeliweza kuvumilia magumu endapo Mungu asingekuwa amempa amani na ndio maana anazungumza kwamba umjue sana Mungu ili uwe na amani kwenye maisha yako. Ukiikosa hii usitegemee hata siku moja kama unaweza kuvumilia kwenye magumu yawayo yeyote na ndio maana hata ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu amani imetoweka ndani mwao kwahiyo msingi mkubwa wa ushindi ni amani pasipokuwa na amani huwezi ukashinda.

2. KUKOSA NGUVU PAMOJA NA MAOMBI

Nguvu huwa ni uwezo wa kufanya jambo ambapo hapa unaweza ukaenda kimwili au kiroho. Lakini ngoja niende moja kwa moja kiroho ambapo unapokuwa unazungumzia Nguvu unakuwa unazungumza habari za ROHO MTAKATIFU.

MATENDO YA MITUME 1:8 
“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Roho mtakatifu huwa ni mwalimu na huwa pia anatusaidia kutuombea mbele za baba kwa kuugua kwa namna kusiko weza tamkika kwa akili za kibinadamu (WARUMI 8:26). Kwahiyo usipokuwa na Roho mtakatifu (ambaye huleta Nguvu ukishampokea) ambaye ndiye atakusaidia uweze kuvumilia magumu ambayo yanakusumbua basi utakuwa na wakati mgumu sana wa kuendelea na safari yako. Katika haya yote lazima uwe na mda wa kusema na Mungu ili uweze kuvumilia na maombi pasipo nguvu za Roho mtakatifu ni kujidanganya ndugu. Ndio maana biblia inazungumza kwamba mengine hayawezekani isipokuwa kwa kufunga na kusali (MATHAYO 17:21) Kwahiyo hautaweza kuvumilia na kumuelewa Mungu mpango wake kukuruhusu upite kwenye Magumu ikiwa hautakuwa na Nguvu pamoja na maombi.

3. KUKOSA MTU WA KARIBU ATAKAYE WEZA KUKUSHAURI KATIKA ,MAMBO MEMA

Kuna watu ambao huwa wanaamini ya kwamba wakiwa pekee yao katika mambo yao basi ndipo wanaweza kukaa vizuri na Mungu wao, ni vizuri siwapingi wala kuwakosoa katika hilo lakini hakuna kitu kizuri katika maisha kama ushirikiano ila inatakiwa watu unao shirikiana nao wawe na nia njema ndani ya mioyo yao na ndio maana tu viungo katika mwili wa Yesu kristo ili kwamba tuweze kusaidizana katika sehemu mbalimbali.

2WAFALME 5;3,9-14 
“Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake, Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, Kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.”

Naamani asingeweza kupata uponyaji endapo kama angekuwa na watu ambao hawakuwa na ushauri mwema juu ya kutii sauti ya mtumishi wa Mungu Elisha kwamba ajioshe mto wa Yordani mda wa siku saba. Kwahiyo katika magumu yako yote unayoyapitia lazma uwe na watu walio wema wanao kuzunguka ili uweze kupata ushauri mwema wa kuweza kuvumilia na kumuelewa Mungu.
Pia lazma uwe makini sana na hao watu wako wa karibu maana pia waweza wakawa kikwazo katika kufikia malengo na makusudi ya Mungu kwenye maisha yako. Kumbuka mke wa Ayubu aliweza kumshauri kwamba aweze kumkufuru Mungu ili afe baada ya kukutana na majaribu magumu sana kwenye maisha yake. Kwahiyo lazma uwe mtu wa kumsikiliza Mungu ndipo utaweza kufikia Lengo ambaloliko mbele yako la kufuata sheria za Mungu na kuvumilia kwenye majaribu na magumu yako.

4. KUACHA KULITII NENO LA MUNGU
Unaposhindwa kufuata maagizo ya Mungu ndipo unaruhusu shetani achukue nafasi ndani ya moyo wako ambapo wewe utafika hatua huwezi tena kufuata njia ya Mungu bali utaongozwa katika njia ya mwili na mara zote mwili Huwa upo kupingana na Roho

WAKOLOSAI 3:5
 
“Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;”

Kwahiyo usipoishi kwa neno la Mungu lazima utazifuata tamaa za mwili na utakuwa ni mtu usiyeweza kuvumilia katika magumu yawayo yoyote maana tayari ndani yako kuna mambo ya mwili yamekutawala kiasi kwamba huwezi kufanya maamuzi yawayo yoyote ya rohoni kwahiyo utaenda kwenye kukata tama.

5. KUKOSA SUBIRA JUU YA MUNGU
Unaweza ukawa umeokoka vizuri na unamjua Mungu vizuri lakini ukakosa subira mbele za Mungu kwahiyo utajikuta unafanya mambo tofauti na namna neno la Mungu linataka uwe.

ISAYA 40:27-31 
“Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie? Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”

Mungu kwa ajili ya watoto wake huwa hawezi akazimia au akachoka kwahiyo ukikosa subira mbele za Mungu utakosa nguvu ya kukuwezesha kushinda kwahiyo lazima uwe na wakati wa kumsubiri Mungu ili uweze kupewa nguvu mpya za kuweza kushinda kwenye maisha yako ya kila siku na kila nyakati unapopita kwenye wakati mgumu kwenye maisha yako.

Lazma tuwe na tarajio kubwa mbele za Mungu ndipo utamuona Mungu anafanya mambo makubwa kwenye maisha yako ya kila siku hata kama unaona wakati unakua mgumu kwako bado kuna tumaini katika kristo Yesu kwamba kuna kushinda katika hilo.
Unapokuwa upo kwenye magumu lazma uwe na uhakika kwamba Mungu bado anaweza akafasha kwenye mambo yak ohayo unayoyapitia ili uweze kushinda kila siku.

MAMBO YANAYOWEZA KUKUPA UHAKIKA WA USHINDI KWENYE MAGUMU NA CHANGAMOTO UNAZO ZIPITIA

1. Mungu huwa hawezi kunyamaza kwa ajili yako maana wewe ni wa thamani sana mbele za Mungu maaana yeye anakutazama kila inapoitwa leo kwenye maisha yako

ISAYA 62:1
 “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo”

Ukitambua kwamba Mungu kwa ajli yako hawezi kunyamaza basi utaishiu kumtendea Mungu mambo mema na utakuwa na uhakika wa safari yako.,

2. Avumiliaye mpaka mwisho ndiye mwenye kuweza kufanikiwa.

MATHAYO 24:13 
“Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.”

Ukifika wakati unajua kwamba mwisho wa jambo ndio kuna wokovu basi utaweza kupata nguvu zaidi ya kuvumilia kwenye magumu yale yanayoumiza moyo wako.

3. Heri mwisho wajambo kuliko mwanzo wake

MHUBIRI7;8 
“Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.”

Ukifika hatua ukaelewa kwamba Mungu huwa anautazama mwisho wako basi utapata uhakika wa kushinda maana tayari Mungu ameweka hatima yako tayari kwa ushindi wako kila siku haijarishi mazingira

4. Ukimjua Mungu ukaanguka hali yako inakuwa mbaya sana

2PETRO2:20-22 
“Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.”

Endapo kama ukaelewa vema kama mtumishi wa Mungu kwamba umekwisha kuokoka na kumjua Mungu alafu ukarudi nyuma yani ukayarudia matapishi, ukazirudia dhambi, ukaendelea kutokumuamini Mungu basi hali yako itakuwa mbaya sana na Mungu atachukizwa na wewe sana na hautaweza kusimama vema

Ndio maana biblia inasema kwamba sisi ni chumvi na inasema endapo ikaharibika yani tukiharibika tutatiwa nini hata tuweze kukolea yani tuweze kuwa na thamani ya kutumiwa kama watumishi wa Mungu kwenye kutangaza Neno la MUNGU

MATHAYO 5:13 
“Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.”

Kwahiyo lazima ujue hayo yatakupa nguvu ya kuweza kushinda kwenye maisha yako kwa kuwa ,mvumilivu mpaka pale Mungu alikusudia uweze kufiika.

HITIMISHO
Mungu akubariki sana mwana wa Mungu kwa kushirikiana nami katika kusoma hili somo ambalo Mungu alikuwa ameliweka ndani yangu kwa ajili ya kanisa ili kanisa liweze kuongeza imani juu ya Utendaji wa Mungu kwenye maisha ya mwanadamu haijarishi mazingira yamekuwa vipi hata kama unaona kutokuweza kuendelea
BADO LIPO TUMAINI KATIKA KRISTO YESU JUU YA UTENDAJI WAKE USIMPE MIPAKA MUNGU YEYE ANAJUA NAMNA YA MKUKUHUDUMIA MWANA WA MUNGU

Kama umebarikiwa unaweza ukawashirikisha na wapendwa wengine katika kristo YESU
MUNGU AKUBARIKI SANA

Ulikuwa nami mpendwa katika kristo Yesu
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email: jackobombwaga@gmail.com


KUSIMAMA IMARA NDANI YA YESU KRISTO (sehemu ya Pili_Final)

Bro Jackobo Utakuwa nami mtumishi katika Kristo Yesu Jina: Bro Jackobo Number: +255766944441 Email: jackobombwaga@gmail.com Blog website: ja...