KUSIMAMA IMARA NDANI YA YESU KRISTO (sehemu ya Pili_Final)


Bro Jackobo

Utakuwa nami mtumishi katika Kristo Yesu
Jina: Bro Jackobo
Number: +255766944441
Email: jackobombwaga@gmail.com
Blog website: jackobombwaga.blogspot.com


Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu?? Pole kwa kuendelea kusubiri sehemu ya pili ya Somo hili kwa mda mrefu toka imetoka sehemu ya kwanza...

Kila jambo na majira yake basi yakiwa ni majira na nyakati ambazo zimekubarika na Bwana, sasa Imempendeza Mungu kwamba wakati huu tuendelee na mfululizo huu wa somo hili. Nikuombe tuende pamoja kwenye hii safari naomba nenda kapitie sehemu ya kwanza ya Somo hili kama uliikosa kwa kubonyeza hapa.πŸ‘‰πŸ‘‰ SEHEMU YA KWANZA

Katika kipengele cha kwanza tuliona utangulizi wa somo, maandiko ya msingi yanayobeba somo letu na tukaona namna ya kuingia ndanj ya Yesu kristo kiundani zaidi. Leo tutaendelea na kipengele cha nne.

4. MAANA YA KUSIMAMA IMARA NDANI YA YESU KRISTO/MUNGU.
Kama nitaendelea kuzungumza juu ya kusimama Imara katika Kristo Yesu pasina kutoa mwelekeo sahihi wa ki maana basj tunaweza kuwa tunatwanga maji kwa kinu. Basi nitatoa maana zisizopungua tatu ili mtu aweze kujitafakari na kujisoma katika kio ya kwamba amekaa kwa namna gani.

Kusimama Imara ndani ya Yesu humaanisha hivi πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

A: Kusimama imara ndani ya Yesu ni hali ya mwamini kuendelea kutembea katika taratibu za Ki Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Yohana 16:13
"Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake."

Roho Mtakatifu ni Mungu kamili kabisa katika nafsi ya tatu ya Mungu kwenye utatu mtakatifu (Holy Trinity) ambaye huyo anajua kila jambo la mwanadamu ambapo mtu hawezi kujificha kwake ambaye Yesu alikuwa anawaambia wanafunzi wake kuwa atakuja huyo ambaye atawaongoza katika njia ya kweli maana alitambua ya kwamba ni kweli wamemkubali lakini bado bila msaada wa Mungu hawawezi kuendelea kutembea au kuishi katika Yeye. Kwahiyo mwamini ili aweze kuishi maisha yaliyo matakatifu katika taratibu zake lazima akae na kujazwa na nguvu za Mungu ambazo hupatikana kwa kuwa na Roho wa Mungu na ndio maana Yesu anawaambia wanafunzi wake kwambaπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Matendo ya Mitume 1:4,8
[4]Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; 
[8]Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. 

Kuna kitu ambacho kama kanisa lazima tukielewe hapa tusije kuchanganya Roho mtakatifu sio Nguvu, Ila yeye ni Mungu ambapo kwa kila mtu anayempokea huwa anakuja nazo Nguvu ambazo hizo nguvu hukaa sasa na huyo mwamini. Kwahiyo Yesu alikuwa akizungumza na wanafunzi wake kuwa kupitia huyo ndipo wataweza hata kuwa na nguvu za kuwasaidia kuwa mawakili wa Siri za Mungu kwakuwa anao uwezo na ndio maana kupitia huo uwezo unaweza kumfanya mtu akaendelea kutembea na Mungu kwenye taratibu zake alizo ziweka anazotaka watu wamuishie ambapo huko ndio kusimama Imara ndani yake. Mwanadamu anapotoka nje ya taratibu za Mungu ni kwamba anakana kwamba yeye hawezi kufuata mambo ya Mungu kitu ambacho hakitamfanya mtu huyo kuwa Imara ndani ya Mungu.

Kwahiyo unahitaji kuwa imara ndani ya Yesu kristo lazima uwe tayari kuziishi taratibu za Mungu anazotaka mwamini aweze kutembea katika hizo. Lazima jifunze Neno la Mungu kwako kibinafsi ndipo utaweza kuelewa kiundani zaidi Mungu anayotaka na sio kusubiri tu mapokeo kutoka kwa viongozi wako wa kidini (Wachungaji, Wainjilisti, mitume n.k) maana kwasasa injili imechakachuliwa kiasi kwamba mtu unahitaji neema ya Mungu kuujua uharisi wa neno la Kweli la Mungu. Tafuta Mungu wa kweli kibinafsi ndugu yangu katika kristo Yesu ndipo utapata usalama kabisa yani.

B: Kusimama imara ndani ya Yesu kristo ni hali ya mwamini kuendelea kukua na kuongezeka
Katika neema ya Mungu ambayo amekwisha kuipokea. 
2 Petro 3:14-18
"Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake. Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele".  

Hapa tunamuona mtumishi wa Mungu petro akizungumza na kanisa juu ya namna watu ambao hawajasimama Imara wanavyoyapotosha maneno ya Mungu akiwataka kanisa kuwa na uvumilivu wa kumngoja Mungu na kumtazamia yeye akitaka wasijitie katika uchafuu wa aina yeyote (Wasiwe na mawaa). Mwishoni anaendelea na kumaliza kuwa kueni katika neema akitaka watu waishike sana ile imani waliyoipokea pasina kudondosha hata nodi moja ya neno La Mungu maana neema ya Mungu ilishafunuliwa kwao yani wakaipokea pasina kuigharamia hiyo neema.
Mtu anapoendelea kuishikilia neema ya Mungu ambao ndio wokovu mkuu anakuwa anakuwa Imara ndani yake kwahiyo lazima tuendelee kuongezeka viwango vya kumuelewa Mungu kwa namna ambavyo ametupatia huu wokovu na kuuishi yani tuendelee kufika kwenye kimo cha kristo Yesu..

Waefeso 4:13
hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; 

Kama ukiishi kwenye neema ya Mungu unakuwa unaendelea kuongezeka mpaka kufikia kwenye kiwango cha ufahamu na nia ya dhati ya Yesu kristo kwenye maisha yako ya kila siku.

C: Kusimama Imara ndani ya Yesu kristo ni hali ya mwamini kuendelea kung'ang'ana na kusimama katika njia ya Mungu licha ya upinzani kuwepo kwenye maisha yake ya kila siku.

Watu wengi sana tumekuwa wepesi sana kumtukuza na kumsifu Mungu pindi tuko nyakati za Furaha na amani huku ukifika wakati wa ukame na changamoto tunamsahau Mungu tuliyekuwa naye wakati wa mwanzo na kuanza kufikiri kana kwamba Mungu ametuacha kumbe yeye amekuwa na sisi wakati wote hata wakati wa Magumu yetu ya kila siku. Kuna wakati ulipaswa utoweshwe uzima kwa magumu hayo lakini uliendelea kuwa hai, lazima ujue ya kwamba  bado Mungu anatafuta uaminifu wako kwake yeye na ndio maana unapita hapo kwahiyo usiogope kabisa. Paulo anasema neno moja hapa chini πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

1 Wakorintho 10:12-13
"Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili."

Kumbe jaribu lolote analolipitia mwamini ni kwasababu ya Mungu mwenyewe ameliruhusu na anajua ya kwamba unaliweza. Kwahiyo lazima uendelee kumshikilia Mungu kwenye nyakati hizo maana Mungu ameweka mlango wa usalama kwenye hilo jaribu. Pale unapo vumilia ndipo sasa unakuwa umekaa imara ndani yake kikamilifu kama anavyotaka. Usikubari kupiga magoti kwa shetani kwasabu ya gumu umepitia kwa mda mrefu maana pale unapofikiri kuwa Mungu amekuacha ndipo Mungu yuko pamoja na wewe anataka kukutoa hapo uwe salama. Usivunjike moyo Mungu anakupenda bado.


5.KWANINI MWAMINI ANAPASWA KUSIMAMA IMARA NDANI YA YESU KRISTO 

A: Kusimama Imara ni mapenzi ya Mungu kwa kila mwamini. Mpango wa Mungu kwa kila mwamini ni kuwa afuate sheria yake na ndio maana kama mwamini lazima utafute kuishi kama Mungu anavyotaka. Ukikataa kuwa imara maana yake umepingana na Mungu kwa maagizo yake.

Mambo ya Walawi 22:31-33 "Kwa hiyo mtayashika maagizo yangu, na kuyafanya; mimi ndimi BWANA. Wala msilinajisi jina langu takatifu; lakini nitatakaswa mimi katika wana wa Israeli; mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi, niliyewaleta mtoke nchi ya Misri, ili niwe Mungu wenu; mimi ndimi BWANA."

B: Kusimama Imara ndani ya Yesu humfanya mtu kuufurahia wokovu wake: Watu wengi wamekuwa kanisani hawana furaha ya kuwepo humo kwakuwa wameruhusu maisha ya aibu ndani yao kiasi kwamba wanaendelea kupata shida na utumishi wao maana dhambi zina walemea hawana hata furaha kabisa. Sasa ukitaka kupata burudiko lazima uwe imara ndani yake na ndio maana Daudi baada ya kuwa amekosea na moyo wake hauna hata furaha akawa anaendelea kumuomba Mungu kwamba amrejeshee furaha ya wokovu wake.πŸ‘‡πŸ‘‡

Zaburi 51:12 "Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi." 

C: Mungu atafanyika Baba kwetu kikamilifu. Mungu anapomuokoa mwanadamu huwa anamfanya kuwa mtoto wake kwahiyo akikufanya mtoto huwa haki zote za Baba anazibeba mwenyewe. πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 1:12 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;"

Huyu mtoto wa Mungu lazima akae katika taratibu za Mungu na ikitokea akatoka katika njia yake ule uwana na kumuamini kwake kunakuwa hakuna maana kabisa. Sasa ukiangalia kanisa la korintho walikuwa watoto lakini walijichanganya kwakuwa na ibada za sanamu na kuingiza mambo mengi mengi machafu ambayo yalimpelekea Paulo kuandaa waraka kwa ajili ya kuwarejesha kwenye msitari na kuwaambia mambo yanayoweza kutokea kwa kutokutii kwao lakini anamaliza kwakuwaambia ili wawe na faida ya Mungu kufanyika Baba kwao lazima wayaache yale yote maovu. Kwahiyo ukiwa imara utayaacha yote na Mungu atakuwa Baba kwako.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

2 Wakorintho 6:17-18 "Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, 
Msiguse kitu kilicho kichafu, 
Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi."


6. MAMBO YATAKAYO NIFANYA NISIMAME IMARA NDANI YA KRISTO YESU
Katika kila jambo ili liweze kusimama katika mpango kamili wa kiutendaji kuna nyenzo kuu za kuzifuata ili kuweza kufanikisha jambo hilo, Vivyo hivyo katika eneo hili la kuweza kusimama Imara ndani ya Yesu kristo kuna vitu/mambo ambayo mwamini lazima ayafuate ili kuweza kukamilisha hali yake ya kuweza kukaa ndani ya Yesu kristo akiwa Imara kabisa. Mambo hayo ni kama ifuatavyo

A: Neno La Mungu
Moja wapo ya jambo la msingi katika mambo ya msingi kwa mwamini ili kuweza kusimama Imara ni kuwa na Neno la Mungu katika uhalisia wake na sio kwenye kupapasa. Mwamini lazima apate neno lake kwenye mafunuo sahihi sana ya Neno lake ndipo ataweza kuyaona matokeo.

Yoshua 1:8  "Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana."  

Mungu alikuwa akizungumza na Yoshua baada ya kumpa nafasi ya uongozi kuwapeleka katika nchi ya Ahadi akimtaka Yoshua kukishika kitabu cha torati (Neno la Mungu). Mungu alitaka akili ya Yoshua ikae kwenye maelekezo yake maana Neno la Mungu huwa linafanya mambo yafuatayo

Neno la Mungu hutoa na kuonyesha njia ya mwamini ambayo anapaswa kuziendea:  kitu kitakachomfanya Mtu ajue hakika mapenzi ya Mungu yalivyo katika eneo hilo.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡
Zaburi 119:105 "Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu." 

Neno La Mungu huleta tabia kwa mtu. Neno la Mungu lina Nguvu ya kutoa na kuleta mambo mapya ya tabia ya Ki Mungu kikamilifu na ndio maana kila mbegu huwa inaleta matunda yafananayo na hiyo mbegu mfano Mbegu ya Embe huleta mti wa Muembe na haiwezekani ikatoa machungwa hata siku moja. Kwahiyo lazima ujikite kwenye Neno lake ili likupe tabia za Ki Mungu ndipo utakuwa salama kabisa kwenye maisha yako. Katika mfano wa Mbegu ambao Yesu aliutoa alionyesha namna Mbegu inaleta matokeo ya kitabia lakini shida inakuwa ni moyo wa mtu ambao ni udongoπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡
Luka 8:11 "Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu."

Neno la Mungu humfanya mtu azaliwe upya kila siku(mara ya pili): Mwamini anapaswa kuwa mpya kila siku na ndio maana maisha yetu ni ya kukua sikuzote kumfikia kristo katika kimo chake cha utakatifu.  Sasa mwanadamu kupitia Neno la Mungu ambayo ndiyo mbegu amefanywa akazaliwa mara ya pili kwa ajili kumfaa yeye aweze kukaa kwenye pendo la Mungu kila inapoitwa leo. Ndio maana hata Petro anakuja kusema kwenye waraka wake kwambaπŸ‘‡πŸ‘‡
1 Petro 1:23 "Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele."

Neno La Mungu limefunga mafanikio ya mwamini: Mungu alimwambia Yoshua kuwa atakapokishika kitabu cha torati na kukiishi na kuwa na tafakari nacho ataweza kufanikiwa kwa kila anachokifanya, kwahiyo katika kuwa Imara ili uweze kufanikiwa lazima uwe umejaa Neno lake ndipo utaweza kufanikiwa lasivyo utashindwa kabisa kuvuka salama.

Neno La Mungu huleta Ulinzi kwa maisha ya mwamini: Watu wengi ili wasipotoshwe na mafundisho mapotofu lazima wawe na Neno la Kweli la Mungu ndani yao pasipokuwa hivyo watapeperushwa na kila upepo wa kila aina, hii ndio sababu hata Yesu alipokuwa anataka kuondoka alikuwa anawaombea wanafunzi wake walindwe na Neno La Mungu maana alijua usalama upo huko. Sasa na mwamini ili aweze kuwa Imara lazima awe na Neno kamili ndani yake litakalo mpa ule ushindi wa kweli.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Yohana 17:11-12,14 "Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu."

Neno La Mungu imebeba nguvu ya makatazo ya Dhambi: Kila mwamini aliyeokoka huwa anaye Roho mtakatifu ambaye hutumia neno la Mungu kama njia ya makatazo katika kuhakikisha huyu mtu anamuishia Mungu wake. Hii ndiyo sababu ilimfanya hata Daudi kuliweka Neno la Mungu moyoni mwake ili aweze kuishi mbali na maisha ya Dhambi kwenye siku zake za maisha akiwepo hapa Duniani.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡
Zaburi 119:11 "Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi."

B: Maombi
Maombi ni njia ya mawasiliano baina ya pande mbili yaani mwamini na Mungu wake. Mwamini akitaka kusimama Imara sasa ndani ya Yesu kristo lazima awe mtu atakaye kuwa na mawasiliano na Mungu maana huko kuna siri nzito za kuweza kumfanya aendelee kusalia katika mpango wa Mungu kama Yeye anavyohitaji.
Haya mawasiliano hayapaswi kuwepo tu pindi mtu atakapokuwa na shida au matatizo bali iwe ni mfumo wa Maisha yake ya kila siku ndipo ataona faida kubwa ya maombi kwenye kuwa Imara ndani ya Yesu kristo. Watu wengi hawaoni matokeo ya maombi yao kwakuwa maombi yao ni ya msimu wa matatizo na sio tabia yao ya kila nyakati. Yesu mwenyewe kila wakati alikuwa akifanya ibada ya maombi kila alfajiri kwaajili ya kuimarisha urafiki wake na Baba.

Luka 22:40-43 "Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu."

Ukiangalia hapo juu utaona kuna mambo ya msingi ya kuondoka nayo ambayo yamefungwa kwenye maombi ikiwa mtu atayaishi

Maombi huwafanya watu kuepukana na majaribu: Yesu alikuwa anawaambia wanafunzi wake waombe wasije kuingia kwenye majaribu, kumbe moja wapo kitu kitakacho wafanya watu wasiingie kwa majaribu ni kupitia kuomba. Hapa Yesu hakumaanisha kwamba wataishi maisha bila majaribu bali hawataweza kuyatii maelekezo ya majaribu maana mara nyingi majaribu huja kutaka kukutoa katika uwepo wa Mungu. Mtu wa Mungu ataendelea kukaa imara katika Hilo kwakuwa maombi yatampa uwezo wa kushinda.

Maombi humsaidia mtu kuyaishi mapenzi ya Mungu hata kama mwili hauko tayari: Yesu mwili wake haukuwa tayari kabisa kuyabeba yale mateso ya msalaba lakini kupitia Maombi aliweza kustahimili. Kwahiyo mlango mwingine wa kuishi mapenzi au matakwa ya Mungu ni kuwa mtu wa Maombi wakati wote.

Kupokea Nguvu za wakati wa Udhaifu wako. Mwanadamu anapokuwa anapitia nyakati Ngumu huwa saikolojia yake iko chini kwenye maamuzi kiasi kwamba biblia inasema anakuwa dhaifu kwa kuwa na nguvu chache. Sasa mtu anapokuwa anaomba anapewa nguvu na ndio maana Yesu alitiwa nguvu ili aweze kuukabili ule msalaba lasivyo ingekuwa shida sana kwake kwakuwa mwili wake ulikuwa hauwezi kabisa na Yeye alikuwa katika mwili huu wa Nyama. Unaweza ukaona hapa πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡ 
Mithali 24:10 "Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache."

Pia kuna umuhimu mkubwa wa mwamini kujieleza mbele za Mungu juu ya uhitaji wake hata kama Mungu anaona na anajua mambo yote. Ni kweli Mungu ndiye anakufanya wewe uwe imara ndani yake lakini usipoonyesha uhitaji wa kumtaka yeye akuhudumie uwe na uhakika hautafika katika ule utimilifu wake wa kweli katika kukaa imara ndani yake.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡
Wafilipi 4:6-9 "Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi."

C: Kujazwa na ROHO MTAKATIFU
Moja ya jambo la msingi kwa maisha ya mkristo ni kuwa na Roho mtakatifu maana pasina huyo hata kama wewe ni mhubiri mkubwa au mwimbaji usipokuwa naye huyo hauwezi kufahamika na Baba maana yeye ndiye alama ya utambulisho wako mbele za Mungu.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Warumi 8:9 "Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake."

Sasa mara nyingi mtu yeyote ambaye amekwisha kuokoka lazima anakuwa na Roho wa Mungu isipokuwa anaweza akawa hajajazwa na Roho mtakatifu na ndio maana hata Yesu alikuwa anawaambia wanafunzi wake wafurahi kwakuwa majina yao yameandikwa mbinguni na kama ingekuwa hawana Roho wake wasingekuwepo kabisa. πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡
Luka 10:20 "Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni."

Sasa kwa upendo wa Mungu kupitia Yesu kristo ndio maana alitaka watu hawa wawe wamejazwa nguvu kwa kumpokea Roho mtakatifu.

Matendo ya Mitume 1:8 "Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.".
Watumishi wa Mungu lazima tujae kiasi cha kuweza kuongozwa na Roho mtakatifu na sio kujiamulia maamuzi kwa uwezo wa Nguvu zetu za kila siku katika maisha Yetu.
   *Soma ezekia 47:1-5*

7.UHUSIANO WA WA KARIBU UTAKAO NIFANYA NISIMAME IMARA NDANI YA YESU KRISTO.
Mwamini lazima ahakikishe maisha yake yako na muda wa kutosha wa kuhusiana na Mungu aliye hai ili aweze kuzifaidia karama za rohoni zitakazo mpa namna ya kuweza kusimama Imara ndani yake. Mtu huyu anapokuwa na muda wa maana na Mungu huwa kuna faida anazipata kama
■ Kuweza kuzipata zile nguvu za Kiroho
■kupata maelekezo ya kiroho ya namna ya kuishi katika usahihi wote
■ Kuwa na uwezo wa kutambua na kuishi kusudi la kiroho la wewe kuwepo.

1 Yohana 5:14-15 "Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.

Yohana anazungumza juu ya kuwa na ujasiri pindi pale unapokuwa una Muendea Mungu na kuamini kwamba unapoomba basi Mungu anafanya, sasa huwezi kuwa na ujasiri kama hautakuwa na uhusiano wa karibu sana kama zaidi ya uhusiano wa mume na mke. Kama vile mahusiano ya mume na mke yalivyo kwamba lazima kila mtu ajue kumpatia mwenzi wake muda wa kutosha na wa maana kabisa vivyo hivyo hata mwamini anapaswa kumpa muda wa maana Mungu wake.

Uhusiano wako wa karibu na Mungu unaweza kujengwa kwa kuwa na muda wa maana kwa namna ifuatayo:-

A: Kuwa na muda maalumu na Mungu
Lazima umpe Mungu kipaumbele kwa kumpatia muda wa kwanza ambapo hapo utakuwa unawasiliana na Mungu kwenye maisha yako ya kuwa mwanafunzi wa Mungu. Muda huu inapaswa kuwepo kabla ya jambo lolote kufanyika ili kuonyesha ule utegemezi wako kwa Mungu wako unaye muabudu na kumuishia. Tunamuona namna mtumishi wa Mungu paulo anavyoliambia kanisa kupitia kwa Timotheo ya kwamba kabla ya yote lazima dua sala na maombezi yafanyike. πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

1 Timotheo 2:1 "Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;"

Pia katika yote tunapata kielelezo kingine cha muda wa maana na Mungu wetu kupitia Yesu kristo Yesu kwa namna alivyoamka alfajiri ili apate muda wa kuomba ambapo nasi yatupasa kufanya hivyo kwa utukufu wa Mungu. Hapa tunajifunza zaidi kushiriki kwa zile ratiba za mtu mmoja binafsiπŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡
Marko 1:35 "Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko."

Haijaishia hapohapo tunaona namna ambavyo wanafunzi wa Yesu walikuwa wanaishi na kukaa katika ratiba za pamoja kwenye muda maalumu kwa ajili ya ibada kitu ambacho kilisaidia wao kuwa na uhusiano wa karibu na baba kwa namna iliyoendelea kuwajenga katika Roho zao. Lazima kama kanisa pia tuwe na nidhamu katika eneo hili kwenye muda wa Ibada ili tujengeke katika yeye.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡
Matendo ya Mitume 3:1 "Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa."

B: Kuwa na Muda wa kutosha
Mwamini anapaswa kudumu sana katika maombi ili maombi yake yapate kujibiwa yaani awe na muda wa utoshelevu. Mfano Yesu aliwataka wanafunzi wake waweze kukesha naye kwenye maombi kwa angalau lisaa limoja ambapo wengi wao wameichukulia kama ndio standard ya mtu mwamini anapaswa kuomba. πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Marko 14:37 "Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja?"

Ingawa watu wapo ambao wameweka hizo taratibu za kusema lazima kuwe na lisaa limoja ila mimi nimekaa nikajifunza nakuona hatupaswi kuishi kwa kukariri bali tuishi kwa maelekezo ya Mungu, Kwahiyo lazima uombe sio kumaliza muda au masaa ulikuwa umeyaweka ili uombe bali omba mpaka usikie ndani ya nafsi yako kuwa umehifadhiwa na Roho mtakatifu. Kwahiyo lazima tuombe pasina kukata tamaa kabisa na tuwe na muda utakao fanya nafsi zetu zirizishwe na kuomba kwetu.

 Luka 18:1 "Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa."

C: Kuwa na Eneo maalumu
Hapa mwamini unashauriwa kuwa na eneo lako binafsi utakalo litumia kwenye kuzungumza na Mungu tena eneo hili inapaswa kuwa eneo lisilokuwa na muingiliano wa watu wengi ili kuto kukutoa kwenye uthabiti wa kuendelea kuwasiliana na Mungu. Tunamuona Mungu alipokuwa anataka kusema na Musa ilimrazimu amtoe kwenye kundi la watu amuite kwenye eneo la utulivu pasina watu ili aseme naye. Vivyo hivyo nasi lazima tuwe na eneo la namna hiyo.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Kutoka 24:12-18 "BWANA akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe. Musa akaondoka na Yoshua, mtumishi wake, Musa akapanda mlimani kwa Mungu. Akawaambia hao wazee, Tungojeeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu; na tazameni, Haruni na Huri wapo pamoja nanyi; kila mtu aliye na neno na awaendee. Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima. Na huo utukufu wa BWANA ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu. Na kuonekana kwake ule utukufu wa BWANA kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli. Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku." 

D: kuwa na mikakati na mpango maalumu kwa ajili ya Mungu.
Kama mwamini lazima uwe na mpango wa kutaka kukutana na Mungu kwakuwa na mikakati dhabiti ya namna gani unaweza kulifikia lengo lako hilo. Inapaswa kama mwamini uwe na ratiba maalumu ya kukutana na Mungu wako kama vile unavyoweka ratiba zako za kufanya kila siku ndipo utaweza kuishi na kutenda kama ulivyokusudia ndio maana Suleiman anasema nasi kupitia mithali kuwa.πŸ‘‡πŸ‘‡πŸ‘‡

Mithali 29:18 "Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria."

E: Fanya Biblia iwe kitabu rafiki kwako
Lazima upate muda wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu kupitia Biblia yako ndipo utajitengenezea Muda wa maana na Mungu wako na kuona faida kwenye maisha yako. Hii itakufanya uwe imara sana lasivyo utapata shida sana.

Yoshua 1:8 "Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana."  

Katika yote hayo tumejifunza juu ya uhusiano wa karibu ndio msingi wako mkuu utakao kuwezesha kutokutoka kwenye uwepo wa Mungu kwenye haya maisha yako ya kila siku.

Mungu akupe neema ya kuendelea kukaa katika uwepo wa Mungu siku zote pasina kuangalia mazingira yako yanakushawishi na kukutaka ufanye maamuzi gani.

Mungu akubariki kwa kuambatana nami toka Mwanzo wa Somo mpaka hapa mwisho.

Ulikuwa nami mtumishi katika Kristo Yesu
Jina: Bro Jackobo
Number: +255766944441
Email: jackobombwaga@gmail.com 
Blog website: jackobombwaga.blogspot.com

2 comments:

  1. Haleluya........
    Mungu akubariki sana Brother, hakika YESU KRISTO BWANA atuwezeshe zaidi kuzidi kusimama imara kudumu katika hilo na kuwa faida kwa ufalme na wote walioridhiwa nao
    Mungu akubariki sana kwa neno na utumishi huu
    Asante

    ReplyDelete
  2. Bwana Yesu akubariki sana mwalimu (Clinton Sanga).

    ReplyDelete

KUSIMAMA IMARA NDANI YA YESU KRISTO (sehemu ya Pili_Final)

Bro Jackobo Utakuwa nami mtumishi katika Kristo Yesu Jina: Bro Jackobo Number: +255766944441 Email: jackobombwaga@gmail.com Blog website: ja...