Utakuwa nami mpendwa katika kristo yesu
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com
Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu?? Karibu Tena kwenye sehemu hii ya pili ambapo ni muendelezo wa somo la Kujikana ndani ya Kristo Yesu ambapo tuliona maana ya kujikana ndani ya Yesu kristo, Tuliona nani alikuwa mwanzilishi wa kujikana tangu asili ambaye ni mfano wetu wa kuigwa tukamalizia na maeneo muhimu mawili ambayo mwamini anapaswa kuonyesha na kuthibitisha kuwa amejikana ndani ya kristo Yesu. Kama hujalisoma somo hilo naomba uende usome sehemu ya kwanza kwa kubonyeza hapa SEHEMU YA KWANZA.
Leo tutaanzia kwenye kipengele cha vipingamizi katika kujikana ndani ya Kristo Yesu.
4. VIPINGAMIZI KATIKA KUJIKANA KWA MWAMINI NDANI YA KRISTO YESU.
Tunapozungumza juu ya Vipingamizi tunaangalia juu ya mambo au vitu ambavyo vinaweza kuleta shida kwa mtu huyu ambaye anataka kujitoa kwa ajili ya kristo vinakuwa vinamrudisha nyuma licha ya yeye kutaka kusonga mbele kwenye kujitoa kwaajili ya Yesu wake aliye muaamini. Watu wamejikuta wanakumbana na vikwazo vingi sana vinavyowafanya washindwe kujidhabihu vizuri katika eneo la utumishi na Utakatifu na utaua.
Vikwazo hivyo ni kama ifuatavyo
A). Upinzani wa ndani ya nyumba ya Mungu/kanisa
B). Upinzani wa nje ya nyumba ya Mungu/kanisa
C). Fedha
D). Msimamo wa kiuaminifu katika mahusiano baina ya jinsia mbili
E). Vyakula
F). Uelewa mdogo wa Mungu unayemuabudu
G). Vyeo vya kiuongozi
A. UPINZANI WA NDANI YA NYUMBA YA MUNGU/KANISA
Hivi vizuizi vinakuwa vinatokana na mazingira ya ndani kwenye nyumba ya Mungu ambayo yanamfanya huyu mtumishi wa Mungu ashindwe kuishi ule utayari wake wa kumtumikia Mungu ambapo ndio kujikana halisi kwa mwamini.
Mathayo 16:21-23
"Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu."
"Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu."
Ukiangalia hapo juu utaona Yesu alikuwa akikemewa na petro kwamba hata pitia mateso lakini Yesu hakumsikiliza Petro bali aliangalia mbele ili kutimiza kusudi lake lililomleta. Tulitegemea kwamba Petro asiwe kikwazo au kumvunja moyo Yesu kutimiza kusudi japo kwa akili ya kibinadamu ilikuwa ni ngumu sana kuelewa ule utumishi ambao ilitakiwa Yesu kuupitia. Hii ndio inatufanya hata nasi kama waamini lazima tuelewe vizuri ni kwa namna gani Mungu ametuita ili tuweze kumtumikia na kama tusipoelewa ndio tunajikuta sasa tunaishia kuvunjwa moyo na watu watu wa karibu au ndani ya nyumba ya Mungu.
Unaweza ukavunjwa moyo na watumishi wa Mungu mfano Mwalimu, mchungaji, mzee n.k lakini usiache kufanya kazi ya Mungu. Wewe hakikisha unamtazama kristo tu kama kielelezo chako katika kumtumikia Yeye.
Kwa namna gani upinzani wa ndani unaweza kuwafanya waamini wakate tamaa??
1. Kuzuiliwa katika huduma na kiongozi wako wa kiroho; usiaangalie ni kwa namna gani kiongozi wako kakuambia au kukukataza kutumika kikubwa jihakikishe uhusiano wako na Mungu halafu uendelee kumuomba Mungu ili akupe namna ya kutumika.
2. Maisha ya dhambi kwa viongozi wa kiroho wanaosimama mbele ya madhabahu; watu wengi wanaosimama mbele ya madhabahu wamekuwa wakiwavunja moyo watumishi wengine kutumika kwa kuwa na maisha mabovu sana. Japo usimfanye mwanadamu akawa ni kielelezo chako kwenye kumtumikia Mungu maana wanadamu watakukatisha tamaa lakini wewe mtazame Yesu na umfuate na sio vinginevyo.
NOTE: HUU UPINZANI WENGI UNAWAINGIZA KWENYE MTEGO KWASABABU YA KUTO KUMUELEWA MUNGU WANAYEMTUMIKIA PAMOJA NA KUSUDI WALILOLIBEBA NDANI YAO.
B). UPINZANI WA NJE YA NYUMBA YA MUNGU/KANISA (WATU WASIO AMINI)
Hapo mwanzoni tumeona upinzani unaopatikana ndani ya nyumba ya Mungu na kumfanya huyu mtu akashindwa kujikana kwaajili ya kristo Yesu, lakini hapa tutaona mambo yanayoweza toka nje ya ya nyumba ya Mungu (wasio Waamini) na kumfanya huyu mtu akarudi nyuma.
Yohana 16:1-3
"Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi."
Yesu aliamua kuwaambia wanafunzi wake juu ya changamoto na upinzani watakao upata kutoka kwa watu wa dini ya kiyaudi ili kwamba wasije vunjika moyo hata siku moja. Na aliwaambia hivyo maana alijua wapo watakao fanya kama kuwaua kabisa wakijua ya kwamba wanamtumikia Mungu lakini kiuhalisia hawako kumtumikia Mungu bali wanafanya kazi ya shetani.
Pale ambapo ukikutana na watu wanakupiga vita juu ya kumtumikia Mungu huko nje usije ukaacha kumtumikia Mungu hata siku moja wewe fanya kazi ya Mungu tu hata kama mazingira ni magumu sana.
Kuna watu huwa wanakataliwa na ndugu na kutengwa na familia kabisa kisa wamemkubali Yesu, sasa hata kama yakikutokea hayo jua tu kuwa ni upinzani wa nje unaotaka kukukwamisha usimuishie Mungu wako uliyekubali kujikataa kwaajili yake, Fanyauwezavyo usiingie katika huu mtego utakuwa salama sana yani.
Note: Watu wamekuwa na urafiki usiokuwa na mipaka kiasi kwamba hawawezi tena hata kuwaambia watu wengine juu ya utumishi wao walio nao. Kwahiyo watu wako wa nje na nyumba ya Mungu lazima uishi nao kwa kwa akili sana ili usije ukapoteza lengo la kuishi. Hakikisha maisha yako mwenyewe ni ushuhuda tosha kwa ajili ya kukurahisisha kuweza kuwahudumia wale walioko nje waujilie ule upendo wa Kristo Yesu.
C. FEDHA
Fedha na dhahabu vyote hivi ni mali ya Mungu mwenyewe (Hagai 2:8) hivi vyote Mungu amempa mwanadamu awe ni wakili juu yake kwahiyo hata kwenye matumizi yake yanahitaji neema ya Mungu sana ili mtu asitoke katika msingi wa Neno lake. Sasa katika kanisa letu la leo tumehama kabisa kutoka kwenye uwakili wa hizo mali tumepewa na Mungu kiasi kwamba tumechagua kuiweka mioyo yetu kwenye mali zetu kwa kuzipa kipaumbele kuliko hata kumpa Mungu nafasi ya kutuongoza. Hapa tunapewa maonyo na mtumishi wa Mungu juu ya fedha.
1 Timotheo 6:10 "Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi"
2 Timotheo 3:1-2 "Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi"
Sasa ukisoma hapo unaona ya kwamba kuwa na pesa sio kitu kibaya ila kuuhamishia moyo wako kwenye pesa na kuzipenda kunakuwa ni mzizi wa mambo mengi mabaya kuweza kutokea maana ukiwa katika hali hiyo unaweza kufanya jambo lolote pasipo hata kufikilia mara mbili juu ya madhara yanayoweza kutokea kwa maamuzi yako.
Ukiwa mtu wa kupenda sana fedha ni ngumu sana kumuabudu Bwana na ndio maana hata maandiko yanatuonyesha kuwepo kwa mabwana wawili ambao ni Fedha na Mungu ambapo haiwezekani ukavitumikia vyote kwahiyo lazima uchague kimoja cha kwenda nacho ndipo utakuwa salama.
Mathayo 6:24 "Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali."
Hii inatuonyesha namna pesa ilivyo na nguvu sana ya kuteka mioyo ya watu kama hawataangalia na kukaa vizuri kwenye nafasi zao. Kwasababu ya fedha kuwa na nguvu ya kushika mioyo ya watu, watu wengi wametupilia mbali ule ujasiri wao na kujikana kwao kwaajili ya kristo Yesu wameanza kutafuta tu pesa. Watu wengi wameacha mambo ya ki Mungu kabisa mfano Kuhubiri injili, kuwepo kwenye makusanyiko ya ki imani wako busy na mambo ya kutafuta fedha na ndio maana ukienda makanisani siku za jumapili utakuta watu wengi sana lakini siku za katikati huwezi kuwakuta watu kwasababu wengi wao wako busy kutafuta pesa wameacha nafasi ya Mungu na hata ndani ya mioyo yao hawajihisi hata Hatia au kukosea kwakuwa fedha zimekuwa Bwana kwao. Mungu atusaidie sana kwenye eneo hili tusije kutekwa mazima tukapotea
NAMNA GANI FEDHA IMEKUWA KIKWAZO KWA WATU KWENYE KUJIKANA KWAAJILI YA KRISTO YESU??
1. Watumishi kuwashikilia watu wenye Fedha kwenye uongozi ingali wanafanya maovu; Hii imekuwa kikwazo sana maana wachungaji wengine wamejikuta wakilitukanisha jina la Mungu kwasababu hiyo maana wanakuwa wameyachagua matumbo yao badala ya kumchagua Mungu wa ibada za kweli.
2. Watu wanadanganya ili wapate fedha: Kitendo cha kukubali kudanganya na kupata fedha ni dhahiri kabisa kuwa umeuacha upendo wa Mungu na kuushika mwenendo usiokuonyesha kujitoa kwako kwa Mungu. Mfano Gehazi alikubali kudanganya ili apate fedha (2wafalme5:21-23).
3. Kuanguka kwenye zinaa (Uasherati na uzinzi) ili kupata fedha: Dunia ya leo imejaa Zinaa sana kiasi kila utakapopita kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali masuala ya ngono yanapewa matangazo makubwa sana kiasi kinawafanya wengi kuanguka kwenye mtego kirahisi lakini wengine wanaingia huko ili wapate fedha ambapo ni jambo la kutisha sana tena sana.
4. Watumishi wengine wanatumia nguvu za giza kwenye huduma zao ili wapate washirika wengi lengo ikiwa ni kupata fedha kutoka kwao:
Wito wangu naomba usikubali fedha ikakutoa kwenye mpango wa Mungu aliokuitia hakikisha unaupa ufalme wa Mungu kipaumbele kwanza kabla ya hizo mali na uchumi unao utafuta na Mungu katika hayo atakuzidishia sana tena sana.
D. MAHUSIANO BAINA YA JINSIA MBILI TOFAUTI
Moja ya maeneo yamekuwa ni changamoto sana kwenye kizazi cha leo ambacho Mungu mwenyewe alikiita kizazi cha zinaa (Mathayo 12:36, 16:4) ni kuwa na uaminifu kwenye uhusiano wanao kuwa nao baina ya jinsi mbili yani mwanamke na mwanaume. Watu wengi wako makanisani lakini uasherati na uzinzi ni kitu cha kawaida sana kwao na wala hata hawaogopi kabisa wanaona tu ni kawaida yani wameizoelea neema ya Mungu kiasi kwamba hata wanapoonywa hawawezi kumtii Roho wa Mungu.
Mungu anataka watu wasiingie kwenye huu mtego wa zinaa kwa namna yeyote lazima wayajue mapenzi ya Mungu ndipo wataweza kushinda lasivyo wataanguka kwa mtego wa adui na ndio maana Suleiman anaseme kwenye Mithali mambo haya hapa
Mithali 6:25-26 "Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate;
Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani"
Mithali 5:15-20 (15-16) "Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako. Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali, Na mito ya maji katika njia kuu?
Baada ya Mungu kusema na vijana wasio na ndoa na kuwaonya juu ya kuwa na uaminifu kwenye eneo hili anasema pia juu ya wanandoa kubaki kwenye kiapo chao na kuwa waaminifu kwa kutokutoka nje ya ndoa zao (Kunywa maji ya birika lako mwenyewe) hii itakufanya kuwa mtu ambaye umejikana kikamilifu sana mbele za Mungu wako lakini isipokuwa hivyo utakuwa wewe haujajikana mbele za Mungu hata kama unaingia nyumbani mwa Mungu".
Unaweza ukasoma maandiko haya kwa faida yako zaidi (1WAKORINTHO 6:9, WAGALATIA 6:7-8).
E. VYAKULA
Watu wanaweza wakashangaa kwa namna gani chakula kinaweza kikamfanya mtu akashibdwa kujikana vizuri mbele za Mungu!! Ila naomba fuatana nami, watu wengi huwa wanajikwaa sana katika eneo la chakula mfano akikosa chakula yuko tayari kumuacha Mungu wake ili alishibishe tumbo lake, wengine wametoa hata rushwa ili wapate chakula chao cha kila siku, wengine walifika wakamnung'unikia Mungu kwasababu ya kukosa chakula
Kutoka 16:2-3 "Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote."
Wana wa Israeli walikuwa wanafikiria chakula walichokiacha misri na kuacha kumtazama Mungu mpaka wakawa wanamlaumu Mungu kwanini aliwatoa misri wakasahau mateso waliyokuwa wanayapata mpaka wakawa wanamlilia Mungu. Kwahiyo kukosa chakula kusikufanye ukamkosea Mungu au ukamtukana Mungu wako hata siku moja bali chagua kumuheshimu Mungu wako.
Tumekuwa na masherehe mbalimbali kwenye kizazi chetu lazima uchague kumtukuza Mungu tu kwenye eneo hili, wengine wameingia kwenye mtego wa kushiriki hata vyakyula vilivyotolewa kwa sanamu/ vyakyula ambavyo vinaleta machukizo mbele za Mungu mfano Pombe n.k. lazima tujifunze kwa mtumishi wa Mungu Danieli namna alivyo azimia moyoni mwake na akapata kibali na kumtukuza Mungu wake kupitia hilo👇👇👇👇
Danieli 1:8 "Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi."
F. UELEWA MDOGO WA MUNGU WAKO UNAYEMUABUDU
Moja ya msingi mkubwa wa upotovu kwa maisha ya mwamini ni uelewa mdogo juu ya Mungu wako, haiwezekani kujitoa kikamilifu hata siku moja kwa Mungu usiyemjua kikamilifu lasivyo utakuwa unapapasapapasa tu kitu kitakacho kupoteza kwenye ramani ya ki Mungu.
Kutoka 32:1-6(1)
Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.
Wana wa Israel walikuwa hawamjui Mungu wao ambaye amewatoa nchi ya utumwa bali walimjua Mussa na ndio maana baada ya Mussa kuchelewa waliamua kuchonga sanamu kitu kilicho mchukiza sana Mungu kwakuwa hawakumpa heshima aliyokuwa amestahili. Watu wengi hawamfahamu vizuri Mungu wanaye Muabudu na ndio maana wanaweza kufanya mambo ya ajabu ajabu tu mbele zake na wengi wapo kwa nyumba ya Mungu lakini hawawezi kujitoa kikamilifu mbele zake.
G. VYEO VYA KIUONGOZI
Kanisa Tulilo nalo kwasasa limekuwa na changamoto sana kwenye eneo hili yani wachungaji wamekuwa wakifanyiana hata mambo ya ajabu, washirika wamekuwa wanachafuana lengo ni kuweza kupata nafasi za kiuongozi kitu ambacho kimewapelekea wengine kutenda dhambi kitu kinachowafanya wawe hawajajitoa kikamilifu mbele za Mungu kama ambavyo anataka Mungu wetu.
Herode alitaka kumuua Yesu kwasababu ya kuhofia kupoteza nafasi yake ya kiuongozi kitu kilicho mfanya akaamua kuangamiza watoto wote chini ya miaka miwili (MATHAYO2:1-18). Jambo kama hili halifai kuonekana kabisa kwa mtu ambaye amekubali kumuamini Yesu kristo kwahiyo jifunze kuondoa wivu utakuwa salama. Ona hapa namna sauli pia alivyoharibikiwa.
1 Samweli 18:6-9 "Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile."
Ukisoma utaona namna Sauli alivyojaa wivu kwasababu ya kuutaka uongozi kiasi alikuwa tayari kumuua Daudi ili asiwe na mpinzani wa aina yeyote kwenye nafasi ya ufalme, Ndugu yangu usije ukaingia kwenye mtego wa kutaka kuwa kiongozi na ukamtukanisha Mungu wako kwakufanya mambo ya ajabu, Rizika na mahali Mungu amekuweka ukae na cheo alichokupa ili jina la Mungu litukuzwe na akuinue kwa wakati wake anaoona kwake unafaa kwako.
Mungu akubariki kwakuwa nami Sehemu hii ya pili ya mfululizo huu. Wa Somo letu hili Zuri, naomba usiache kufuatilia muendelezo wa sehemu ya tatu na ya mwisho kwenye somo letu hili, naamini utapata kitu cha kukupa hatua ya kiroho zaidi
Ulikuwa nami mpendwa na mtumishi katika kristo Yesu
Jina: Bro Jackobo
Namba: +255766944441
Email: Jackobombwaga@gmail.com
Blog: jackobombwaga.blogspot.com

No comments:
Post a Comment