Utakuwa nami mpendwa katika kristo yesu
Name: Bro Jackobo
Phone: +255766944441
Email; jackobombwaga@gmail.com
Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu?? Karibu Tena kwenye sehemu hii ya tatu na ya mwisho ambapo ni muendelezo wa somo la Kujikana ndani ya Yesu ambapo tuliona maana ya kujikana ndani ya Yesu kristo, Tuliona nani alikuwa mwanzilishi wa kujikana tangu asili ambaye ni mfano wetu wa kuigwa tukaona na maeneo muhimu mawili ambayo mwamini anapaswa kuonyesha na kuthibitisha kuwa amejikana ndani ya Yesu kristo Yesu katika sehemu ya kwanza halafu tukasoma sehemu ya pili ambapo tuliangalia vipingamizi katika kujikana kwa mwamini mbele ya Mungu wake. Kama hujayasoma masomo hayo naomba uende uyasome ili upate mtiririko mzuri. Unaweza kubonyeza hapa ili usome ππππ
Leo Tutaanzia kwenye kipengele cha madhara kwa kanisa kushindwa kujikana kikamilifu kwaajili ya kristo Yesu.
5. MADHARA KWA KANISA KUSHINDWA KUJIKANA KWAAJILI YA YESU KRISTO.
Mungu wetu ni wa utaratibu sana amabaye hawezi kumlazimisha mtu kumfuata bali anatamani kila mtu amfuate kwakuwa amependa kumfuata japo yeye Mungu sio kama mwanadamu ambaye ameweka uongozi wake usiwe wa mfumo wa kidemokrasia tu bali ameuweka uongozi wake wa theoklasia (Theocracy) ambapo ana utaratibu wake anaotaka tuufuate ambao una maelekezo ya kila kitu tunachotakiwa kukifanya na akaweka kwamba tusipofuata kuna madhara yatakayo tokea.
Sasa kanisa lazima likubali kufuata taratibu zake mwenyewe lasivyo madhara yatatupata kama ifuatavyo hapa chiniππππ
A. Kutokujibiwa kwa maombi yetu
B. Kukosekana kwa matendo makuu ya Mungu
C. Kupotea kwa kibali na heshima mbele za Mungu
A. KUTOKUJIBIWA MAOMBI
Maombi ni mawasiliano ya pande mbili ambapo huwa mwamini anamuelezea yule anayemuamini juu ya yale yanamsibu na muaminiwa kutoa majibu kwa anayemuamini juu ya kile alichokiweka mezani. Kwahiyo maombi ni mchakato wa njia mbili ambapo lazima pande zote zipate muitikio kutoka kwa upande mwingine juu ya hoja moja inayowaunganisha ili kujenga uhusiano wa karibu sana "Intimacy".
Kwasababu ya kanisa kutokuwa na uhusiano mzuri na Mungu yani kushindwa kujitoa kikamilifu kwaajili ya Yesu kristo, mambo mengi yamemfanya Mungu azibe sikio lake lisiweze kusikia yale ambayo wanahitaji kwasababu hakuna lengo moja linalowaunganisha la kimahusiano. Sasa Mungu ndio maana anataka watu wake wote wajitoe kikamilifu na kama hawatajitoa wanakuwa wameikataa sheria yake na ndio maana anakuja kusema ya kwambaπππ
Mithali 28:9 "Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo."
Pia ukifuatilia biblia utagundua wana wa Israel pale walipokosea mara nyingi waliingia katika mikono ya adui hata kupewa adhabu na Mungu mwenyewe. Sasa kipindi cha nabii Amosi wana wa Israel walikuwa wamekosea kiasi wakawa wanaabudu mpaka sanamu huku bado wakitaka kutaka kumfanyia Mungu ibada huku hawajajikabidhi kwa Mungu kikamilifu mpaka ikafika Mungu. Anakuja kufoka na kuwaambia maneno hayaππππ
Amosi 5:22-23 "Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu."
Kutoa kwao sadaka na kumfanyia Mungu nyimbo za shangwe za kuoyesha furaha yao kwa Mungu hakukuwa na maana kabisa mpaka Mungu akawa anawaambia wamuondolee nyimbo zao maana zimekuwa kelele kwakuwa mioyo yao haikuwa kwake kamili. Kwahiyo ukitaka Mungu akusikie lazima ujitoe kikamilifu mbele zake lasivyo utakuwa unajidanganya na utakuwa unapoteza muda wako. Hii inakuja kuthibitisha kile Mungu anataka kiuhalisia wakeπππ
Yohana 9:31 "Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo."
Sasa lazima pia uwe na moyo wa kutafakari kikamilifu sana na kwaakili ambayo imetulia sana kuelewa hili. Mungu amesema mwenyewe kabisa kwenye maandiko yake kuwa pale ambapo mtu anachagua kuishi katika dhambi huwa dhambi inamfarakanisha na Mungu na hata yale mambo anayokuwa anayaomba Mungu hawezi kuyajibu wala Mungu hawezi kuwaokoa maana dhambi inakuwa ni kiambaza kinacho watenganisha nyie na Mungu wenuππππ
Isaya 59:1-2 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; ]lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."
B.. KUKOSEKANA KWA MATENDO MAKUU YA MUNGU.
Kanisa inapaswa kuwa ni sehemu ambapo madhihirisho makubwa ya uwezo wa Mungu kwa matendo makuu kuonekana lakini kwasasa imekuwa nii kitu ambacho ni adimu sana kwasababu watu wengi hawako thabiti sana mbele zake ili na yeye aweze kuyaonyesha matendo yake kwa kanisa. Kizazi hiki kimekuwa kina ukaidi sana hakiko tayari kabisa kujitoa kikamilifu kwaajili ya kristo kitu ambacho kinaleta mapooza ndani ya Nyumba ya Mungu na Mungu kumfanya anyamaze kabisa. Yesu alizungumza wazi kabisa kuwa kizazi hiki kitatafuta ishara lakini hakitapata kwasababu ya movu yao katika maandiko kadhhaa πππ
Mathayo 16:4 "Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake."
Mathayo 12:38-39. "Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona."
Sasa ukitaka kuelewa vizuri unaweza ukarudi nyuma ukaona namna Gideoni alivyokuwa anashangaa kwamba walisimuliwa matendo makuu ya Mungu lakini kipindi chao hakuona yale matendo makuu ya Mungu ila ameona namna ambavyo taifa la Israel likiwa liko chini ya kongwa la utumwa wa wamidiani mpakka akawa anajiuliza wewe Mungu ikoje hapa lakini hakuwa amezingiatia kuwa taifa la Israel lilikuwa limeingia katika dhambi ndicho kitu kikawafanya wasiyaone matendo makuu ya Mungu.πππ
Waamuzi 6:1,13 "Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA; BWANA akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani."
(Unaweza ukasoma pia waamuzi 2:10-15)
Kwahiyo mlango mkuu wa kanisa kutokuona matendo makuu ya Mungu ni kuto kujitoa kikamilifu kwa Yesu mwenyewe maana yeye ndiye mwenye matendo makuu, lazima tukubali kumfuata na kuacha yote kwaajili ya Yesu kristo Yesu.
C. KUPOTEA KWA KIBALI NA HESHIMA MBELE ZA MUNGU.
Mungu anapo liona kanisa lake likiwa limepoteza mwelekeo anaoutaka kwa kutokujitoa kwake mbele zake huwa anacho kifanya anaondoa mambo makuu mawili ambayo ni muhimu sana ambayo ni
A. Heshima
B. Kibali
Ufunuo wa Yohana 2:5 "Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu."
Ukisoma hapo juu unaona Yesu anazungumza kupitia kinywa cha Yohana kuwa lazima ukumbuke ulipoanguka ili utubu na usipofanya hivyo anakuja kuondoa kinara (Kibali na heshima) ambayo alikuwa amekupatia ili ubaki wewe mwenyewe maana haujafuata njia zake. Kama alivyokuwa ametaka. Hii kitu ndiyo ilimfanya pia hata petro kusema hiki kituππ
1 Petro 5:6 "Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;"
Kifupi ni kuwa kama ukinyenyekea (Umejitoa kikamilifu mbele za Mungu) yeye atakuinua kwa wakati wake( Yani atakupa Heshima). Kiufupi kama usipofanya hivyo uwe na uhakika atakupa aibu kabisa kwakuwa mkono wake hautakuwa juu yako na shetani atakuwa na uhalali wa kufanya kile anachokitaka kwenye maisha yako ya kila siku.
Naomba tuangalie japo kwa kifupi juu ya kibali ili kuweza kuelewa uzuri wa kuwa nacho kutoka kwa Mungu.
KIBALI
Mithali 8:35-36 "Maana yeye anionaye mimi aona uzima, naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, nao wanichukiao hupenda mauti."
Mambo muhimu kuhusu kibali
• Hii ni hali ya kupokelewa au kukubaliwa kufanya jambo au kupewa ruhusa ambayo sio watu wote wanapewa bali ni kwa wale waliochaguliwa tu.
• Pia, Kibali humaanisha kuonyeshwa wema, Yani Mungu anakutendea mema ambayo hata wengine huwa wanatamani kama wangeyapata lakini wameyakosa kwasababu ya namna Mungu ametaka mwenyewe.
• Pia hii ni hali ya kupewa upendeleo na Mungu
Mithali 12:2 "Mtu mwema atapata upendeleo kwa BWANA; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye"
Lazima uelewe kuwa kibali huwa kinatafutwa na huwa kinatunzwa kwahiyo kwa kujitoa kwako kikamilifu mbele zako mbele za Mungu kutakufanya upate hicho kibali cha Mungu lakini kama hautafuata matakwa yake utakipoteza kabisa.
MAMBO YA KUKUSAIDIA KUTUNZA KIBALI CHAKO KWA MUNGU
A. Jifunze kuwa na nia safi kabisa ndani yako kila inapoitwa leo
Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye."
1 Wakorintho 10:31 "Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. "
B. Jitahidi kufanya Mema mbele za Mungu
Mwanzo 4:5-7 "bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde."
C.Okoka kwa kumaanisha kwelikweli
D. Kuwa mtu wa Ibada.
Matendo ya Mitume 16:25-26 "Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa."
6. MAMBO YA KUFANYA ILI KULISAIDIA KANISA KUMAANISHA KUJITOA KWAKE.
Mungu wetu ni mwaminifu sana ambaye ametupa maarifa ya kuweza kutusaidia kumaanisha kujitoa kwetu. Kwahiyo kuna baadhi ya mambo ambayo yanaweza kutusaidia kumaanisha kujitoa kwetu kwa Mungu wetu. Mambo yenyewe ni kama ifuatavyo
A. Kumjua Mungu
B.kuwa rafiki wa Neno la Mungu
C. Kumpenda Mungu na mambo yake yote
D. Kuchagua uaminifu na utii
E. Kuwa mtu wa Ibada, Maombi na kutenga muda wa maana na Mungu wako.
A. KUMJUA MUNGU
Moja ya jambo la kumsaidia mwamini kuweza kumaanisha kujitoa kwake ni kumjua Mungu vizuri ili kwamba kwenye kuamua kwake kujitoa anaelewa kwanini ameamua kuambatana naye. Kiufupi nguvu ya kujua inauwezo ndani yake wa kuambatanisha. Huwezi kuambatana na mtu usiye mjua wala huwezi kumuamini kwahiyo ukimjua Mungu utaambatana naye na utamuamini kwakuwa unaelewa kila kitu chake.
Ayubu 22:21 "Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia."
Mtu anapomjua Mungu huwa amani kwake sio kitu cha kuuliza wala kufikiria maana wakati wote anakuwa ana uelewa wa nini anakifanya. Kwahiyo hata kama akiamua kuambatana na Mungu hata yakija magumu hayawezi kumtoa kwenye msitari wa kuendelea kuambatana na Mungu wake na ndio maana Daudi anasema πππ
Zaburi 119:165 "Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza."
Sasa ukimuangalia mtumishi wa Mungu paulo anaeleza namna ambavyo amejitoa kwa kristo Yesu na kuyaona mengine yote kuwa kama mavi, lakini anatamani kumfahamu Mungu wake vizuri kwa kutokutumia haki yake mwenyewe bali kwa imani ipatikanayo katika kristo Yesu kitu kitakachomfanya aweze kumshika Mungu wa mbinguni kiukwelikweli na kuweza kuambatana naye siku zote.πππ
Wafilipi 3:9-10 "tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;"
B. URAFIKI WA KWELI NA NENO LA MUNGU
Neno La Mungu huwa linatoa mwongozo wa namna ya kuishi katika maisha ya kila siku. Mtu anapokuwa rafiki wa Neno la Mungu kila hatua atakayokuwa anaiamua Neno litampa mwongozo na kumfanya aweze kuamua kikamilifu kujitoa kwaajili ya Yesu kristo.πππ
Zaburi 119:105 "Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu."
Mungu ndiye pumnzi na uhai wetu na ndio maana hata kipindi cha Yoshua alimsisitiza kuishika sheria yake kila wakati ili kupitia hiyo imuongoze kwenye maamuzi kwakuwa toka asili Neno la Mungu ndio msingi wa ki maongozi kwa mtu yeyote ambaye amekubali kumfuata Munguπππ
Yoshua 1:8 "Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana."
Mungu siku zote anachokitaka kwa kanisa lake ni ule moyo wa kuwa tayari kusikiliza Maneno yake na kuyatenda na kuhakikisha tunaishi katika hayo. Katika Neno ya Mungu tunapata kuwa salama na ndio maana hata Suleiman alipokuwa ameandika mithali kuna sehemu alisema hiviπππ
Mithali 4:20-22 "Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako;
Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote."
Ukijiuliza ni kwanini mtumishi wa Mungu huyu alisema jambo kama hili unagundua kwamba alikuwa akitamani watu wasikilize mahusia ya Mungu (Neno La Mungu) ambalo hilo unakuwa unamzungumzia Yesu kristo mwenyewe (Yohana 1:1-5) ambapo anatamani tumshike yeye yaani tujitoe kikamlifu kwaajili ya Mungu wetu maana katika yeye tutakuwa hai ikiwa tutamkimbilia. Unaweza ona namna ambavyo hata paulo alisema na watu wa Athene alipowakuta wakiabudu kwa Mungu asiyejulikana na akawatambulisha Mungu anayejulikana na kuwaambia kuwaπππ
Matendo ya Mitume 17:28 "Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.
Ikiwa Uhai unapatikana kupitia Yesu kristo kwahiyo lazima tuwe na urafiki na Neno la Mungu ndipo tutaweza kujikuta tumeweza kulishika Neno La Mungu kikamilifu kabisa na kujikana kwaajili ya kristo Yesu. Jambo lingine mambo mengi tunayaweza kwasababu tumekaa ndani ya Yesu kikamilifu kwahiyo nguvu ya uwezesho wa kujitoa na kujikana kwetu huwa mara nyingi tunapewa kama zawadi tu na Mungu mwenyewe kupitia Kristo Yesu. Ndio maana hata Yesu alizungumza na wanafunzi juu ya kukaa ndani yake ili waweze kuzaa matunda yani kiufupi uwezo wako wa kujikana kikamilifu kwaajili ya kristo Yesu unatokana na Yesu mwenyewe (Urafiki wa kweli na Neno la Mungu).ππ
Yohana 15:5-6 "Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea"
C. KUMPENDA MUNGU NA MAMBO YAKE YOTE.
Mambo mengi huwa tunaweza kuyafanya ni kwasababu Mungu ametuwezesha lasivyo vitu vingi tungeshindwa kuvifanya (Wafilipi 4:13, 2timotheo 4:17). Sasa kwasababu mambo yote tunawezeshwa na yeye ni jambo moja Mungu analolitafuta kwetu ambalo kila wakati aangetamani tuweze kuishi katika njia hiyo ambayo ni Upendo na ndio maana katika kuzitaja amri yeye alitupatia amri moja kuu inayobeba kila kitu ambayo ni upendo.
Mathayo 22:36-40 "Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii."
.
Nimekuambia kuwa unapaswa kumpenda Mungu na mambo yake yote kwasababu kupitia Upendo ndipo utaweza kufanya maamuzi yaliyo sahihi ya kuamua kuambatana na Mungu kwenye maisha yako na kujikataa mwenyewe kabisa, hii ndio sababu hata ukiingia kusoma agano jipya ndipo unaona msisitizo wa mitume ulikuwa juu ya kufanya vitu kwa upendo mfano kwa habati ya utoaji (2wakorintho 9:7). Pia pale utakapo kuwa umempenda Mungu hata kama utapitia magumu hautakata tamaa kumuishia Mungu utajikuta kila kitu kwako ni amani maana yupo Mungu akupaye amani.
Zaburi 119:165 "Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza."
D. CHAGUA UAMINIFU NA UTII
Uaminifu ni hali ya kitabia ambapo mtu anachagua kusimama katika makubaliano, ahadi, wajibu na mahusiano pasina kuangalia upande wa pili hata kama yale mambo yanamuumiza.
Wakati
Utii ni kitendo cha kusikiliza, kukubali na kutenda kulingana na maagizo, sheria au mapenzi ya mamlaka halali, kwa hiari na heshima.
Sasa haya mambo mawili yaani uamini na utii lazima ukubali kuambatana navyo maana katika hivyo Ndipo kuna ufunguo wa kubaki katika mshikamano. Kuna wakati lazima wewe uweke dhamira ya ndani ya kutaka kujikataa kwaajili ya Kristo Yesu ili Mungu aweze kukupa hiyo neema ya kuweza kujidhabihu kweli kweli na ndio maana samweli alimwambia sauli kuwaπππ
1 Samweli 15:22-23 "Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme."
E. IBADA, MAOMBI NA MUDA WA MAANA NA MUNGU.
Maana Ya Ibada
Neno Ibada linaweza kutafsirika kwa namna mbili ukitumia maneno ya kigiriki cha biblia(Kiyunani) ambayo ni "Proskuneo" na neno "Latreia"
"Latreia": humaanisha Huduma ya ibada, kumtumikia Mungu ambpo sasa Huhusisha maisha ya kujitoa kwa Mungu, si matendo ya nje tu bali mpaka utu wako wa ndani kabisa.ππ
Warumi 12:1 "Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana."
"Proskuneo": humaanisha Kusujudu, kuinama kwa heshima na unyenyekevu. Hii Inaonyesha mtazamo wa moyo na mwili mbele za Mungu.ππ
Yohana 4:24 "Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli."
Pale kanisa/mwamini anapochagua kuwa chombo cha ibada huwa wakati wote Mungu anakuwa anafanya kazi pamoja naye, kitu kitakachomsaidia yeye mwenyewe kuendelea kujitoa kwa Mungu wake aliye muita na kumuokoa. Ibada siku zote inakuwa inaambatana na Maombi ambapo lazima utafute mda mzuri wa kuzungumza na Mungu wako ili akupe maelekezo ya namana ya kuishi kitu kitakachokusaidia kuwa salama na kujitoa kikamilifu mbele zake.
Jambo ambalo lilimfanya Yesu aweze kujitoa kikamilifu mbele za Mungu ni ule utayari wake aliokuwa anamfanyia Mungu ibada, pia alikuwa ni mtu wa maombi na alitafuta muda wa maana usiokuwa na vurugu za aina yeyote ambapo na sisi tunapaswa kufuata msingi huo lasivyo tutapotea pasina kujua.πππ
Marko 1:35 "Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko."
Luka 22:39 "Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye."
Mungu akubariki kwa kuambatana nami katika mfululizo wote wa tatu katika somo hili Mungu aliliweka ndani yangu
Kama una swali au sehemu hujaelewa unaweza ukawasiliana nami kupitia mawasiliano hapo chini.
Ulikuwa nami mtumishi katika kristo Yesu
Jina: Bro Jackobo
Number: +255766944441
Email: jackobombwaga@gmail.com




